Kuna kitu kimoja nimekuwa nakiona kila ninapokuwa nawashawishi watu kununua bidhaa au huduma fulani. Wale watu ambao wanaonekana kama hawataki kununua, wanakuwa wabishi na wenye vikwazo mbalimbali, huwa wanakuwa ndiyo wanunuaji wazuri sana wa chochote unachouza.
Watu hawa huwa wanaanza na ubishi na vikwazo kama njia ya kukupima wewe muuzaji. Wanakuwa wanataka kuona ni kwa kiasi gani unajiamini wewe mwenyewe na kuamini kile unachouza ili nao waweze kupima umuhimu wa kile unachotaka kuwauzia.
Mteja wako anataka sana kukuona wewe ukijiamini na kuamini kile unachouza. Na atahakikisha anapima hilo kabla hajanunua.
Kuna wakati mteja anaweza kuja na pingamizi la kubuni tu, ambalo siyo kweli, halafu anakusikilizia unalichukuliaje pingamizi hilo, kama utakubaliana nalo anajua huamini kweli kwenye kile unachouza. Na kama utaendelea kutetea kile unachouza na kuonesha mifano inayopinga pingamizi lake, anaamini na kununua.
Wakati mwingine mteja anataka kuona kama wewe binafsi unatumia kile unachouza na kimekusaidia kwa kiasi gani. Kama unauza kitu ambacho hutumii, au hakuna mtu wako wa karibu unayeweza kumshauri atumie, mteja anakuwa na wasiwasi juu yako na kile unachouza.
Jiamini sana wewe mwenyewe na amini sana kwenye kila unachouza. Kama unakosa imani hizo mbili, usijaribu kuingia kwenye biashara, utashindwa kabla hata hujaanza.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,