Kuna viashiria viwili ambavyo ukiviona kwa mtu, unajua kabisa lazima atafanikiwa, haijalishi anaanzia wapi au anafanya nini.
Na viashiria hivyo vinapokosekana kwa mtu, basi unajua anasukuma tu maisha, hakuna namna anaweza kufanikiwa.
Kiashiria cha kwanza ni UHITAJI AMBAO MTU ANAO. Kama mtu anakihitaji kitu kweli, kwa namna ambayo hakuna kinachoweza kumrudisha nyuma, basi lazima mtu huyu afanikiwe. Mwandishi mmoja amewahi kusema kama mtu atayataka mafanikio kama anavyoutaka hewa anapokuwa amezama kwenye maji, basi dunia haiwezi kumzuia asifanikiwe. Kuwa na uhitaji mkubwa sana wa kufanikiwa, usikubali kikwazo chochote kisimame kati yako na mafanikio yako. Jipe tamko kwamba utapata unachotaka au utakuwa ukiwa unakitafuta. Na kamwe usirudi nyuma kwenye hilo.
Kiashiria cha pili ni KAFARA AMBAYO MTU ANATOA. Mafanikio yanahitaji mtu utoe kafara, tena siyo utoe kitu cha kawaida, bali utoe kitu ambacho unakipenda sana. Huwezi kuendelea na maisha uliyozoea kuishi halafu ukafanikiwa. Huwezi kufanya kile ambacho kila mtu anafanya halafu ukafanikiwa. Acha kujidanganya, kufanikiwa kunahitaji wewe utoe kafara. Mwandishi mmoja amewahi kusema kinachomzuia mtu kufanikiwa ni kile anachokipenda sana, kile anachojiambia hawezi kukiacha. Ukishaweza kuacha hicho, safari yako ya mafanikio ni nyeupe kabisa. Jiambie kwamba upo tayari kutoa chochote ili kufanikiwa, na fanya hivyo kweli na kwa hakika utafanikiwa.
Rafiki, ukiviona vitu hivyo viwili kwenye maisha ya mtu, jua kwa hakika mtu huyo atafanikiwa. Ukiviona vitu hivyo viwili kwako, jua utafanikiwa. Na kama vitu hivyo havipo kwako, jua tu unasukuma siku, hakuna namna utafanikiwa.
Kama umejichunguza na kugundua huna vitu hivyo viwili, chukua muda kuvitengeneza. Kwanza jiulize ni nini hasa unachotaka kwenye maisha yako, ambacho upo tayari kukifia, hilo ndilo linakuwa hitaji lako kuu. Pili jiulize ni kitu gani unachopenda sana kwa sasa ambacho hakikufikishi kule unakotaka kufika, kisha kiache mara moja. Inaweza kuwa ni starehe, inaweza kuwa ni ulevi, inaweza kuwa ni mambo ya kijamii, inaweza kuwa ni uvivu na mengine, bila kuacha mara moja, hutaweza kupiga hatua.
Jua unachotaka na lipa gharama, hakuna kitakachoweza kukuzuia kufanikiwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,