“We don’t abandon our pursuits because we despair of ever perfecting them.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 1.2.37b

Tunayo siku nyingine mpya nw nzuri sana kwetu wanamafanikio,
Siku bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UKAMIKIFU NI ADUI WA KUCHUKUA HATUA…
Kama unasuburi mpaka kila kitu kikamilike ndiyo uanze kuchukua hatua, unajichelewesha kufanikiwa.
Kama huchukui hatua kwa sababu kila kitu hakijakamilika, hujajitoa kweli kufanikiwa.
Watu wengi wamekuwa wanatumia ukamilifu kama kichaka cha kuficha madhaifu yao mengine.
Wanajiambia hawawezi kuanza kwa sababu kuna vitu fulani bado hawajakamilisha,
Cha kushangaza hakuna siku wanakamilisha na hivyo hawaanzi kamwe.

Rafiki, kama unataka kufanikiwa, lazima uchukue hatua,
Na wakati sahihi wa kuchukua hatua ni sasa, hata kama kila kitu hakijakamilika,
Kwa sababu haitakuja kutokea siku ambayo kila kitu kitakuwa kimekamilika kama unavyotaka.

Asubuhi ya leo, hebu orodhesha vitu vitatu ambavyo ulijiambia utaanza kuvifanya mwaka huu lakini bado hujaanza, bado unaendelea kuahirisha na kusema hujawa tayari au mambo hayajakamilika.
Kisha anza leo kufanya vitu hivyo.
Ndiyo, leo hii anza, anza kwa hatua yoyote hata kama ni ndogo kiasi gani.
Kwa sababu safari moja huanzisha nyingine,
Na kama zilivyo sheria za mwendo za Newton, kitu kilichosimama kinaendelea kusimama na kilicho kwenye mwendo kinaendelea na mwendo.
Kama utaendelea kusubiri utabaki hivyo hivyo,
Lakini kama utaanza kuchukua hatua, utaendelea kuchukua hatua.

Je unataka kubaki hapo ulipo au kupiga hatua zaidi?

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuchukua hatua kwa pale ulipo sasa, hata kama kambo hayajakamilika. Anza leo yale yote ambayo umekuwa unaahirisha kufanya.
#UkamilifuNiSumu #AnziaHapoUlipoSasa #SafariMojaHuanzishaNyingine

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1