“Many words have been spoken by Plato, Zeno, Chrysippus, Posidonius, and by a whole host of equally excellent Stoics. I’ll tell you how people can prove their words to be their own—by putting into practice what they’ve been preaching.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 108.35; 38

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo,
Ni siku bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari MILIKI MANENO YAKO…
Kusema ni rahisi, kila mtu anaweza kufanya hivyo,
Lakini njia pekee ya kumaanisha kile unachosema ni kumiliki maneno yako.
Na unayamiliki maneno yako kwa kuweka kwenye matendo yale unayosema, kufanya kile unachohubiri.
Usiwe mtu wa kusema A na kufanya B,
Bali unachosema ndiyo unachopaswa kufanya.

Haijalishi maneno unayosema umejifunza kwa nani, yatakuwa yako kama utayaweka kwenye mayendo ya maisha yako.
Kuishi yale unayohubiri kunakupa kujiamini wewe mwenyewe na hata wengine kukuamini pia.
Kuishi yale unayohubiri kunakuondolea hali ya kukwama na kujikuta njia panda, usijue kipi sahihi cha kufanya.
Kitu sahihi kwako kufanya ni kile unachosema, jiwekee msukumo wa kufanya hicho na utaweza kupiga hatua zaidi.

Kama kila mmoja wetu angeishi yale anayosema,
Kama kila mmoja wetu angetumia mwenyewe ushauri anaowapa wengine,
Basi dunia ingekuwa sehemu bora sana ya kuishi.
Changamoto nyingi tunazopitia zinaanzia pale maneno na matendo yanapopishana.
Usikubali hilo liendelee kwako,
Miliki maneno yako, kwa kuhakikisha maneno na matendo yanaendana.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kumiliki maneno yako kwa kuyaweka kwenye matendo.
#FanyaUnachohubiri #TekelezaUnachoahidi #UsiweNaMaishaYaAinaMbili

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1