Kushindwa hakutokei mara moja, siyo ajali.

Kushindwa ni matokeo ya tabia ambazo mtu anakuwa amejijengea na kuzirudia rudia kwa muda mrefu.

Hakuna mtu anaamka siku moja na kujikuta kwenye madeni makubwa, bali ni tabia ambayo inatengenezwa kidogo kidogo na baadaye inakuwa kubwa.

Hakuna mtu anaamka siku moja na kujikuta ana afya mbovu, ni matokeo ya mtindo wa maisha ambao mtu anakuwa ameuishi kwa muda mrefu.

Hivyo basi, badala ya kusubiri ushindwe ndiyo ujiulize imekuwaje ukashindwa, pitia kila aina ya tabia ulizonazo na jiulize zina mchango gani kwenye maisha yako.

Kila ambacho unakifanya, kitafakari kwa kina kinakupeleka wapi.

Ninachotaka kukuambia ni kwamba baadhi ya vitu unavyofanya kila siku ndiyo vinatengeneza kushindwa kwako. Hivyo kama utajua mapema na kuchukua hatua, utaweza kuzuia kushindwa kabla hakujatokea.

Kama unaweza kutengeneza kushindwa wewe mwenyewe, basi pia unaweza kutengeneza ushindi wewe mwenyewe. Muhimu ni kujua zipi tabia sahihi kwako kutengeneza na zipo tabia zisizo sahihi unazopaswa kuzivunja na kisha kufanyia kazi kila siku kwenye maisha yako.

Kushindwa ni tabia, kagua tabia zako kuhakikisha hazitengenezi kushindwa kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha