“The founder of the universe, who assigned to us the laws of life, provided that we should live well, but not in luxury. Everything needed for our well-being is right before us, whereas what luxury requires is gathered by many miseries and anxieties. Let us use this gift of nature and count it among the greatest things.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 119.15b

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana tuliyoiona leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari ISHI VIZURI, SIYO KWA ANASA.
Tunachohitaji ili tuwe na maisha mazuri ni vitu vichache sana, na tayari tunavyo, vinatuzunguka popote pale tulipo.
Kinachotutesa ni anasa tunazotaka kuwa nazo.
Pale tunapowaona watu wana kitu fulani na kujiambia na sisi lazima tuwe nacho, hapo ndipo tunapovuruga maisha yetu.
Tunaishia kujiingiza kwenye utumwa wa madeni au kazi nzito ili tu tutimize tamaa yetu ya anasa.

Kama wastoa, tunapaswa kujua yapi muhimu kwa maisha yetu na kuhangaika na hayo, na yale yasiyo muhimu tusiyape nafasi ya kutusumbua.
Lakini hii haimaanishi tusiwe na mali wala utajiri, unaweza kuwa na mali na utajiri utakavyo, lakini tu usiwe mtumwa wa mali na utajiri huo.

Wengi wamekuwa wanasumbuka sana na hizi tamaa za anasa, kutaka vitu ambavyo hawawezi kuvimudu, ili na wao wasipitwe au wasionekane wako nyuma.
Kama ambavyo mtu mmoja amewahi kusema; ‘watu wanatumia fedha ambazo hawana (mikopo), kununua vitu ambavyo hawavihitaji (anasa), kuwaridhisha watu ambao hawajali’

Kumbuka unachopigania kwenye maisha yako ni uhuru na utulivu, usikubali chochote kiingili hayo muhimu.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuzingatia yale muhimu na kutoruhusu anasa zikusumbue.
#NidhamuUadilifuKujituma #AfyaUtajiriHekima #KaziUpendoHuduma

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1