Kulijua tatizo kwa undani ni nusu ya kulitatua.
Watu wengi wanateseka na matatizo kwa sababu hawajatumia muda wao kuyajua kwa undani.
Hivyo wanayaparamia, na kila hatua wanayochukua inazidi kufanya tatizo kuwa kubwa zaidi kuliko kulitatua.
Hivyo unapojikuta kwenye tatizo, hatua ya kwanza kabisa ni kujua kwanza chanzo kikuu cha tatizo hilo, kile chanzo ambacho ukikikabili na kukifanyia kazi basi tatizo hilo linatoweka kabisa.
Huu ndiyo ule mzizi hasa wa tatizo, ambao ukiukata, tatizo linakauka. Sasa wengi wamekuwa wanahangaika na matawi ya matatizo, wakikata tawi moja, tawi jingine linaota tena. Wanajikuta kila wakati wapo kwenye hali ya kutatua tatizo lisiloisha.
Katika kulijua tatizo kwa undani, tuanze na matatizo ambayo siyo matatizo, yaani unakuwa unajiambia una tatizo, kumbe huna tatizo.
Na kubwa ni hili, kama una tatizo, ambalo fedha inaweza kulitatua, basi wewe huna tatizo, bali ni huna fedha, hivyo pata fedha zaidi na kisha tatua chochote kinachokukwamisha.
Kwa sehemu kubwa, yale tunayojiambia ni matatizo ni kwa sababu tu hatuna fedha. Hata tafiti zinaonesha, migogoro mingi kwenye ndoa na hata mahusiano ya kawaida huwa inaanzia kwenye eneo la fedha.
Sisemi kwamba fedha ndiyo suluhisho la kila tatizo, bali kwa sehemu kubwa, fedha inatatua matatizo mengi, na kutengeneza mengine pia. Hivyo pata fedha, tatua yale matatizo yanayohusiana na fedha na weka nguvu zako kutatua yale ambayo fedha haziwezi kutatua.
Kwa kuwa sehemu kubwa ya maisha yetu inaguswa na fedha, matatizo mengi pia yanatokana na kutokuwa na fedha za kutosha, hivyo kama tukiweka nguvu kwenye kuongeza kipato chatu zaidi ya tulichonacho sasa, moja kwa moja matatizo mengi yanayotusumbua yanapata jawabu yenyewe.
Jua kila tatizo unalopitia kwa undani, na kama fedha zaidi zinaweza kutatua tatizo unalopitia sasa, basi jua huna tatizo, bali ni huna fedha. Pata fedha zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,