Unapokuwa unaweka mipango, fikiri mambo makubwa, usijiwekee ukomo wowote ule katika kufikiri kwako. Kwa sababu wote tunajua fikra zetu ndizo zinazoumba uhalisia wetu.
Unapokuwa unachukua hatua, anza kidogo, pale unapoweza kuanzia sasa, usisubiri mpaka uweze kuchukua hatua kubwa. Kwa sababu wote tunajua hatua ndogo ndogo zinazojirudia rudia ndizo zinazozalisha matokeo makubwa sana.
Mfano, unapotaka kupanda mlima mkubwa na mrefu, unafikiri makubwa kwa kujiona ukiwa kwenye kilele cha mlima ule. Na unapochukua hatua ya kupanda mlima huo, unapiga hatua moja baada ya nyingine, ni hatua hizo ndogo ndogo zinazokufikisha kwenye kilele cha mlima.
Hivi ndivyo maisha yako yanapaswa kwenda kama kweli unataka kufanikiwa, unapofikiri, fikiri makubwa, unapoanza kuchukua hatua, chukua hatua ndogo ndogo.
Mambo haya yote mawili yapo ndani ya uwezo wako, kwa sababu hakuna anayekuamulia ufikiri kwa namna gani, hivyo kama utaamua kufikiri kidogo jua ni wewe mwenyewe. Pia hakuna anayekupangia uchukue hatua kiasi gani, kama utajiambia unasubiri mpaka uweze kuchukua hatua kubwa utakuwa unajichelewesha wewe mwenyewe.
Amua sasa kufanikiwa kwa kufikiri makubwa na kuchukua hatua ndogo ndogo. Usikubali kukwama popote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,