Dunia inabadilika kwa kasi kubwa,

Kadiri sayansi na teknolojia inavyokua, ndivyo kazi nyingi zinavyozidi kupotezwa kwenye soko la ajira.

Na hata baadhi ya biashara zinapotezwa kabisa na ukuaji wa teknolojia.

Tumekuwa tunaona jinsi ambavyo watu wanasoma na kukosa ajira, jinsi ambavyo makampuni yaliyokuwa maarufu zamani kwa kuzalisha bidhaa fulani yanavyopotea kabisa pale soko linapobadilika.

Hali hii inaleta wasiwasi kwa watu wasijue ni ujuzi gani wanaoweza kujijengea ambao hautaondolewa na ukuaji wa teknolojia.

Ni rahisi kuona kwamba teknolojia ina nguvu ya kuondoa kila aina ya kazi au ujuzi. Mfano mzuri ni maroboti yanayokuja kwa kasi sasa, ambayo yanaweza kufanya kila kitu, kujibu simu, kutumwa, kucheza muziki, kuendesha magari na mitambo, kuhudumia watu na hata kufanya upasuaji kwenye mwili wa binadamu.

Swali ambalo wengi tumejiuliza je ni ujuzi gani uliobaki ambao hauwezi kuondolewa na ukuaji wa sayansi na teknolojia?

Na hapa na kwenda kukupa jibu; JINSI YA KUUZA.

Jinsi ya kuuza ni moja ya ujuzi ambao hauwezi kamwe kuondolewa na ukuaji wa teknolojia. Ujuzi huu hauwezi kupitwa na wakati kamwe.

Kama kuna watu duniani, wenye mahitaji, basi ujuzi wa kuuza unazidi kupata nguvu zaidi.

Ujuzi huu hauwezi kupitwa na wakati kwa sababu mauzo yanahitaji ushawishi. Ni watu wachache sana ambao wanatoka na kwenda kununua kitu kwa hiari yao, wengi inabidi washawishiwe kununua, hata kama kitu wanakitaka kweli.

Hakuna roboti linaloweza kumshawishi mtu kununua kitu ambacho anafikiri hakihitaji, hiki ni kitu ambacho binadamu pekee anaweza kukifanya.

Hivyo popote ulipo, jijengee uwezo wa kuuza, jijengee ushawishi mkubwa, amini kwenye kile unachofanya na usione aibu kuwakabili wengine ili wakubaliane na wewe.

Jifunze jinsi ya kuuza na kamwe hutolala njaa, kwa sababu ukiwa na mikakati na mbinu bora za mauzo, utaweza kuuza kitu chochote kwa mtu yeyote, kama unakiamini kweli kitu hicho na unajua kinakwenda kumsaidia yule unayemuuzia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha