“First practice not letting people know who you are—keep your philosophy to yourself for a bit. In just the manner that fruit is produced—the seed buried for a season, hidden, growing gradually so it may come to full maturity. But if the grain sprouts before the stalk is fully developed, it will never ripen. . . . That is the kind of plant you are, displaying fruit too soon, and the winter will kill you.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 4.8.35b–37

Ni siku mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tumaipata nafasi hii nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari SIYO KWA AJILI YA MAONESHO…
Jifunze kutokuwaruhusu watu wakujue sana na kujua mambo yako ya ndani.
Kwa sababu kadiri watu wanavyojua mambo mengi kuhusu wewe, ndivyo unavyokaribisha matatizo mengi pia.
Na hata kama mambo yako yatajulikana na wengine, basi siyo kwa haraka kama wengi wanavyofanya.

Chukua mfano wa mazao tunayopanda.
Unapanda mbegu, inajificha ardhini kwa muda fulani bila ya kuonekana,
Na hata inapoonekana inakuwa ndogo, ambayo haina matumizi yoyote kwetu.
Kidogo kidogo mche unakua na baadaye kutoa mazao ambayo tunayavuna.
Fikiria kama ungekuwa unapanda mbegu leo na kesho yake inachomoza na kutoa mazao, je mmea huo ungepata nafasi ya kuwa na maisha?

Kwenye zama hizi za mitandao ya kijamii, ambapo ni rahisi sana kuanika mambo yako, wengi wamekuwa wanashindwa kujizuia na kuanika kila kitu, halafu wanashangaa kwa nini mambo yao hayaendi.
Mtu ameanzisha biashara hata mteja mmoja hana tayari ameshasambaza habari kila mahali.
Mtu amechukua shamba hata kuliandaa bado tayari ameshasambaza habari na picha kila mahali kwamba yeye ni mkulima.
Kinachotokea ni wengi wanafaidi tu maonesho, lakini hawafaidi kwenye kile wanachofanya.

Unapoanza kufanya kitu chochote, kipindi cha mwanzo ni cha kuweka kazi na siyo maonesho, ni kipindi cha kujificha kama mbegu iliyopandwa.
Na kadiri unavyoweka kazi, utazalisha matokeo mazuri ambayo yatawafanya watu waone wenyewe na siyo wewe kupiga kelele.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufanya kile ulichochagua kufanya na siyo kuwa na maonesho. Siku ya kutoruhusu kila mtu ajue kila kitu kuhusu wewe.
#AchaManenoWekaKazi #MafanikioSiyoMaonesho #UsikaribisheMatatizoKwaMdomoWako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1