Chochote ulichonacho sasa, kuna siku hutakuwa nacho,
Kazi uliyonayo sasa, kuna siku hutakuwa nayo.
Biashara uliyonayo sasa, kuna siku hutakuwa nayo.
Mali ulizonazo sasa, kuna siku hutakuwa nazo.
Marafiki ulionao sasa, kuna siku hutakuwa nao.
Na hata mahusiano ya karibu uliyonayo sasa, kuna siku watu hao hutakuwa nao tena, na hutaweza kuwaona tena.
Huu ndiyo ukweli wa maisha lakini hua tunajaribu kujisahaulisha. Huwa tunajisahau na kuona chochote tulichonacho tutaendelea kuwa nacho kama tunavyotaka.
Na hii ndiyo inawaandaa watu kwa mshtuko na kuangushwa, pale kile walichokuwa wanakitegemea sana kinapoondoka huku wakiwa hawana maandalizi.
Kwa kujua ukweli huu wa maisha, kuna hatua mbili za kuchukua;
Kwanza ni kutumia vizuri kitu wakati unacho, hapa hakikisha hujutii iwapo kitaondoka, hakikisha umekitumia kwa kadiri unavyoweza kukitumia.
Mbili ni kujiandaa pale ambapo unachotegemea sasa hutakuwa nacho tena. Usipende maisha yakushangaze, badala yake kuwa na maandalizi sahihi kwa chochote unachotegemea sasa, ukijua kuna wakati hutakuwa nacho.
Tumia vizuri ulichonacho sasa, maana siku na saa inakuja ambapo hutakuwa na kitu hicho tena.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,