#TANO ZA JUMA #37 2019; Elimu Ya Kitaa, Amri Kumi Za Biashara, Mambo 68 Unayopaswa Kujua Kufanikiwa Kwenye Biashara, Wakati Sahihi Wa Kuanza Kuomba Mkopo Benki Na Mauzo Siyo Faida.

Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye makala ya TANO ZA JUMA la 37 la mwaka huu 2019. Katika juma hilo tumejifunza kwa kina mambo muhimu unayopaswa kujua ili kuweza kuanzisha na kukuza biashara katika zama hizi zenye ushindani mkali.

Juma hilo la 37 tumejifunza kutoka kitabu kinachoitwa Street Smarts: An All-Purpose Tool Kit for Entrepreneurs kilichoandikwa na waandishi na wafanyabiashara wawili ambao ni Norm Brodsky na Bo Burlingham. Norm na Bo wana uzoefu wa muda mrefu katika kuanzisha na kukuza biashara, na kupitia kitabu hiki wametushirikisha uzoefu wao katika biashara.

street smarts.jpg

Karibu tupate elimu halisi ya biashara kutokana na uzoefu wa wale waliokaa kwenye biashara kwa muda mrefu.

#1 NENO LA JUMA; ELIMU YA KITAA.

Kuna elimu nyingi ambazo tunazipata hapa duniani, lakini mkazo tumekuwa tunaweka kwenye alimu ya darasani kwa sababu tunapomaliza elimu hiyo kwa ufaulu, tunapewa cheti kinachoonesha kwamba tumefuzu. Lakini elimu hiyo ya darasani imekuwa haina matumizi makubwa kwenye maisha halisi tunayokwenda kukutana nayo.

Eneo ambalo elimu ya darasani haiendani kabisa na uhalisia wa mtaani ni kwenye biashara. Mambo mengi kuhusu biashara yanayofundishwa darasani hayaendani na uhalisia. Na hata wale wanaopata nafasi ya kupata elimu ya shahada ya uzamivu kwenye biashara (MBA) bado mambo mengi wanayojifunza darasani hayana uhalisia mtaani.

Ndiyo maana unapoingia kwenye biashara, kama unataka kufanikiwa na kuvizuka changamoto mbalimbali zitakazokukabili, basi unahitaji elimu ya kitaa, elimu ya uzoefu kutoka kwa wale waliopo kwenye biashara na pia kujifunza kutokana na changamoto unazopitia mwenyewe.

Ni muhimu kuwa na kocha au menta anayekuongoza kwenye biashara yako, ambaye anakupa ushauri na mambo muhimu unayopaswa kujifunza kuhusu biashara yako.

Norm Brodsky ambaye tunakwenda kujifunza kupitia kitabu cha juma hili, anatuambia kwamba menta wake kibiashara alikuwa baba yake, ambaye alikuwa mfanyabiashara. Anasema wakati baba yake anakwenda kuuza, alikuwa akiambatana naye na hivyo alipata nafasi ya kujifunza kwa uzoefu halisi. Kuna mambo mengi aliyojifunza kwa baba yake ambayo hakuwahi kujifunza shuleni au sehemu nyingine yoyote, na baadhi ya mambo hayo ametushirikisha kama ifuatavyo;

Moja; Mara zote fanya mauzo mazuri yenye faida kubwa. Ni muhimu sana kuzingatia faida kuliko mauzo. Hili ni somo ambalo wengi huwa hawalielewi, wanakazana kuuza na kuja kujikuta wakiwa kwenye hali mbaya kifedha kwa sababu mauzo mengi wanayofanya yanakuwa hayatengenezi faida.

Mbili; Hakikisha mteja wako ni mtu ambaye anaweza na yupo tayari kulipia kile unachomuuzia. Usikazane kuwa na wateja wengi, badala yake kazana kuwa na wateja bora. Kama wateja ni wasumbufu kulipa usiendelee kufanya nao biashara.

Tatu; Usijinufaishe kupitia wengine. Kwa sababu mtu hajui au haelewi usitumie mwanya huo kujinufaisha zaidi huku ukimuumiza yeye. Kuwa mwaminifu na mwadilifu mara zote. Kuwa mtu wa haki mara zote.

Nne; Fanya maandalizi na usiwe na wasiwasi. Unapokuwa na jambo lolote kubwa linalokuja mbele yako, hupaswi kupoteza muda wako kuwa na wasiwasi kuhusu jambo hilo. Badala yake unapaswa kufanya maandalizi sahihi na kuwa tayari kulikabili. Mambo mengi tunayokuwa na wasiwasi nayo na kuyahofia kwenye maisha huwa hayatokei kama tunavyofikiri.

Tano; Kuna dola milioni moja chini ya viatu vyako, wajibu wako ni kuzitafuta na kuzichukua. Hili ni jibu ambalo Norm alikuwa analipata kwa baba yake kila alipokuwa anamwambia hajui afanye nini. Akimaanisha kwamba fursa zipo nyingi mno, ni mtu kuamua kuchukua hatua na kufanikiwa.

Sita; Usipoomba hupewi. Wote tunajua kauli inayosema ombeni nanyi mtapewa, hii siyo tu kwenye dini na imani, bali ni kauli iliyo kweli kwenye kila eneo la maisha. Kama kuna kitu chochote unachotaka kutoka kwa wengine, basi unapaswa kuomba, unapaswa kuuliza. Kama utakaa kimya, hakuna atakayejua unataka nini na hivyo hutapata chochote unachotaka. Lakini pia unapaswa kujua siyo kila unachoomba utakipata.

Haya ni masomo mazuri sana kuhusu biashara na maisha kwa ujumla, ambayo nina uhakika hukuwahi kupata nafasi ya kujifunza ulipokuwa shuleni. Hii ndiyo elimu ya kitaa, maarifa unayoyapata mtaani, kupitia uzoefu wa wengine na uzoefu wako binafsi. Unapoingia kwenye biashara, elimu ya aina hii ni muhimu sana kwa mafanikio yako, ipe kipaumbele.

#2 KITABU CHA JUMA; MAMBO 68 UNAYOPASWA KUJUA KUFANIKIWA KWENYE BIASHARA.

Juma la 37 la mwaka 2019 tunajifunza kupitia kitabu kinachotupa mafunzo halisi ya biashara kutoka kwa wafanyabiashara wazoefu. Mafunzo haya siyo rahisi kuyapata kwenye mfumo rasmi wa elimu au ushauri mwingine unaotolewa na wengi.

Norm Brodsky na Bo Burlingham kwenye kitabu chao kinachoitwa STREET SMARTS, wametupa mafunzo haya muhimu ambayo tukiweza kuyatumia tutapiga hatua sana kwenye biashara zetu.

Kitabu hiki kina sura 17 na mwisho wa kila sura kuna mambo manne muhimu ya kuondoka nayo na kwenda kuyafanyia kazi. Kwenye uchambuzi huu nakwenda kukushirikisha mambo hayo manne kutoka kwenye kila sura na hivyo tunapata jumla ya mambo 68 muhimu tunayopaswa kujua ili kufanikiwa kwenye biashara.

Karibu ujifunze mambo haya 68, uyaelewe na kuyatumia kwenye biashara yako.

 1. Usiruhusu hisia zako zikuongoze kufanya maamuzi kwenye biashara, itakuwia vigumu kufikia malengo yako kwa sababu utafanya maamuzi mabovu.
 2. Hakikisha unauelewa mzunguko wa fedha kwenye biashara yako na kujua mapema ni wapi fedha zinazoingia kwenye biashara yako zinatoka.
 3. Ondokana na dhana ya kukazana kuuza pekee na tengeneza dhana ya kuikuza biashara kwa ujumla. Mauzo yawe yenye faida kwa biashara.
 4. Jifunze kutegemea na kutambua mabadiliko yanayotokea kwenye biashara yako kwa kuielewa vizuri biashara hiyo. kuchukua hatua kabla ya mabadiliko ndiyo njia ya kuyakabili.
 5. Wale wanaong’ang’ana ndiyo wanaoshinda. Kuwa king’ang’anizi na karibisha kushindwa. Hivyo ndivyo unavyokuwa mfanyabiashara bora.
 6. Unajifunza kwa kuacha kutengeneza sababu za mambo kutokea na kuangalia ndani yako ni makosa gani umeyafanya yanayoletea mambo kwenda vibaya. Ukiwa mtu wa kutafuta sababu au kulaumu wengine, hujifunzi.
 7. Kufokasi na nidhamu ni muhimu kuliko kuziona na kuzitumia fursa. Kama huwezi kufokasi na kuwa na nidhamu, haijalishi ni fursa gani umezipata, hazitakusaidia. Lakini unapaswa kuwa tayari kubadilika kulingana na hali inavyokwenda.
 8. Suluhisho la changamoto unazopitia liko mbele yako. Unahitaji kujua jinsi ya kutambua suluhisho hilo na kulitumia.
 9. Ni vizuri kuwa na washindani kwenye biashara kwa sababu hao wanasaidia kutengeneza na kuelimisha soko. Kuwa kwenye biashara ambayo haina ushindani kabisa kunakupa gharama kubwa ya kutengeneza na kuelimisha soko.
 10. Kama ndiyo mara yako ya kwanza kuingia kwenye biashara, ni bora kujenga biashara yako kuanzia chini kuliko kununua biashara ambayo imeshakuzwa. Unajifunza mengi unapoanzia biashara chini kabisa. Na biashara yoyote unayonunua, huwa ina matatizo yake, ambayo hutayajua mpaka utakapoinunua.
 11. Mchanganuo wako wa kwanza wa biashara unapaswa kuwa rahisi na unapaswa kuuandika kwa ajili yako na siyo kwa ajili ya wawekezaji au taasisi za kifedha. Mchanganuo wa biashara ni njia ya wewe kuielewa biashara yako.
 12. Muda wako ni wa thamani kuliko fedha, unapaswa kuwa makini usipoteze muda wako, kwa sababu ukishapotea hupati tena.
 13. Kabla hujawaomba watu wawekeze kwenye biashara yako, unapaswa kujua ni kiasi gani cha fedha wapo tayari kukiwekeza. Pia unapaswa kujua ni vigezo gani wanavyotumia katika kuwekeza ili uweze kuwaandalia vigezo hivyo.
 14. Anza mapema kutengeneza mahusiano na watu wa benki au taasisi nyingine za kifedha kabla hujahitaji kupata fedha. Mahusiano hayo yatakusaidia pale unapokuwa unahitaji fedha.
 15. Watu wa beki ni wafanyabiashara kama wewe, utoaji wa fedha ndiyo biashara yao na wafanyabiashara ndiyo wateja wao. Wachukulie kama ambavyo ungependa wateja wako wakuchukulie wewe na utaweza kupata kile unachotaka kutoka kwao.
 16. Unapomuuzia mteja bidhaa au huduma kwa utaratibu wa kufanya malipo baada ya kupokea unachomuuzia, hapo ni sawa na kumkopesha mteja wako fedha. Usihesabu ni mauzo mpaka pale utakapokuwa umelipwa.
 17. Kila unapoanzisha biashara mpya, fuatilia mauzo yako na faida ghafi ya kila mwezi kwa kuandika na mkono mpaka pale unapokuwa umeelea vizuri namba hizo mbili za biashara yako. Hapa usitumie programu ya kompyuta wala kitu kingine chochote, andika kwa mkono wako mwenyewe.
 18. Tafuta namba moja ambayo itakuwa inakupa picha ya mwenendo wa biashara yako kila wakati. Namba hiyo inakupa uhalisia na uwezo wa kutabidi mwenendo wa biashara yako hata kama hujapata ripoti kamili ya biashara hiyo. kila biashara ina namba yake, ijue ya kwako.
 19. Mauzo mengi mara nyingi humaanisha mzunguko mdogo wa fedha. Tambua mahitaji ya fedha ya biashara yako kabla hujafika wakati ambapo unahitaji fedha halafu huna. Unapokuwa na maandalizi mazuri inakusaidia pale unapokuwa na uhitaji.
 20. Elewa hesabu ya mapato kabla ya riba, kodi, uchakavu na madeni (EBITDA) na tumia hesabu hii kupima ukuaji wa biashara yako pamoja na thamani yake, badala ya kutumia mauzo pekee.
 21. Kusikiliza ni sehemu muhimu sana wakati wa majadiliano ya kibiashara. Utaweza kupata dili nzuri kama utakuwa msikilizaji mzuri na kuelewa upande wa pili unataka nini hasa. Kaa kimya na sikiliza, kuna mengi ambayo watu wanasema kwa maneno na vitendo.
 22. Unapoenda kwenye majadiliano usiende ukiwa na mawazo yako juu ya upande wa pili, mara zote chukulia upande wa pili unajua kuliko wewe, hivyo kuwa msikilizaji mzuri.
 23. Jijengee tabia ya kuhoji kile unachokiona kwa nje na kuchimba ndani kujua ni nini hasa kinachoendelea. Usiridhike haraka na kile unachokiona kwa nje.
 24. Kwenye majadiliano ya ushindani, dili nzuri ni ile ambayo inauacha kila upande ukiwa hauna furaha kidogo. Kwa kifupi dili nzuri ni ile ambayo inaleta ushindi kwa kila upande na pia kila upande unakuwa umepoteza kitu fulani.
 25. Siri ya mafanikio kwenye mauzo ni kuishinda hofu yako ya kuuliza. Kama huulizi huwezi kupata kile unachotaka.
 26. Huwezi kujua soko halisi la biashara yako mpaka pale utakapoingia kwenye biashara hiyo. Unaweza kuwa na mipango mizuri sana kabla ya kuingia kwenye biashara, lakini unapoingia uhalisia unakuwa tofauti.
 27. Hakuna sehemu ya soko la biashara inayodumu milele, wateja wanabadilika na mahitaji yao yanabadilika pia. Kadiri unavyokwenda na biashara yako unapaswa kuyanusa mabadiliko hayo na kubadilika kabla hujachelewa.
 28. Sifa yako ndiyo mali yenye thamani sana kwenye biashara yako na washindani wako wanachangia sana kwenye kuitengeneza sifa yako. Linda sana sifa yako na ya biashara yako, ukishapoteza hiyo umepoteza kabisa biashara yako.
 29. Unakuwa kwenye wakati mzuri kibiashara ukiwa na wateja wadogo wengi kuliko kuwa na wateja wakubwa wachache. Ukiwa na wateja wakubwa wachache ambao ndiyo unawategemea kwa kila kitu, wanakuwa wanakumiliki wewe, mmoja akiacha kufanya biashara na wewe biashara yako inatetereka. Lakini unapokuwa na wateja wadogo wengi, mmoja akiacha bado unakuwa nao wengine.
 30. Kuonesha kuna nguvu kuliko kueleza. Unapokuwa unamshawishi mteja mpya kufanya biashara na wewe, tumia muda mwingi kumwonesha ni namna gani anakwenda kunufaika kuliko kumweleza.
 31. Hakuna kitu muhimu kitakachoweza kukusaidia kupata wateja kwenye biashara yako kama kusikiliza. Unaposikiliza kwa umakini unaelewa mahitaji halisi ya wateja wako na hivyo kuweza kuwapa kile ambacho wanahitaji kweli, ambacho hawawezi kukikataa.
 32. Usiwe mtu wa kupunguza bei ili tu kupata wateja kwenye mali au nafasi ambayo huitumii. Mfano una gari ambalo unakodisha kwa elfu 50 kwa siku, na kwa wastani unapata watu kwa siku 3 za wiki, ni rahisi kuona kwa zile siku ambazo hupati mtu wa kukodi gari hiyo, akijitokeza mwenye elfu 30 unamkodishia. Lakini hilo linaua soko lako, wale wateja halisi wanapokuja kugundua unakodisha kwa bei ya chini zaidi, hawatatoa tena ile ya mwanzo. Hivyo hata kama biashara ina nafasi iliyo wazi, usipunguze bei ili kuijaza, badala yake kazana kupata wateja sahihi.
 33. Kubakiza wateja kwenye biashara yako ndiyo ufunguo wa ukuaji wa biashara hiyo. Kama kila wakati unahitaji kutafuta wateja wapya wa biashara yako, haiwezi kukua. Kadiri wateja wengi wanavyoendelea kuwa na wewe, ndivyo biashara inavyokua. Njia bora ya kubakiza wateja kwenye biashara yako ni kujenga nao mahusiano bora.
 34. Njia bora ya kutengeneza mahusiano mazuri na wateja wako ni kuwasaidia kwa kuwafundisha kuwa wanunuaji wazuri kwa kuwafundisha kwa kina kuhusu biashara yako. Kadiri mteja anavyoijua biashara kupitia wewe, ndivyo anavyokuamini na kukutegemea wewe kama mshauri wake wa karibu.
 35. Jijengee tabia ya kuwachukulia wateja wa zamani kama ndiyo wateja wapya wa biashara yako. Ni kawaida kwa wafanyabiashara kutoa huduma bora kwa wateja wapya ili warudi tena na kutoa huduma za kawaida kwa wateja wa zamani. Wewe chukulia kila mteja wa biashara yako kama ni mteja mpya na utaweza kudumu nao kwa muda mrefu.
 36. Kadiri biashara yako inavyokua, ndivyo unavyopoteza nafasi ya kuwa karibu na wateja wa biashara hiyo. Tengeneza mpango wa kukupa nafasi ya kukutana na wateja wako mara kwa mara, kuna mengi unajifunza kutoka kwa wateja wako kuliko unavyojifunza kutoka kwa wasaidizi wako wa kibiashara.
 37. Wateja hawapendi kujiona kwamba wanachangia wewe kuwa na maisha ya anasa, hivyo epuka sana kuwafanya wateja kujisikia hivyo. Achana na maisha ya maonesho, weka nguvu zako kwenye kuwahudumia wateja wako na kukuza biashara yako.
 38. Jenga tabia ya kuongeza bei kidogo kidogo kadiri muda unavyokwenda badala ya kusubiri kuja kuongeza bei kwa kiwango kikubwa kwa wakati mmoja. Kumbuka kila unapoongeza bei kwa kiwango kikubwa, kuna wateja utakaowapoteza. Badala ya kusubiri miaka mitano ndiyo uje kuongeza bei mara moja, ongeza bei kidogo kidogo kila mwaka.
 39. Biashara yako ndiyo mali yenye thamani kubwa sana kwako. Usiruhusu thamani yake kupotea kwa kuacha faida ipotee. Ni rahisi sana kwa faida kupungua kadiri biashara inavyokuwa, kuwa mlinzi hodari kwenye hilo.
 40. Kuwa makini na sheria unazoweka kwenye biashara yako. zinaweza kuwa sheria ambazo zinawafanya wasaidizi wako kufanya maamuzi mabovu au kutoa huduma mbovu kwa wateja. Hakikisha unaacha mwanya wa mfanyakazi kufanya maamuzi ya kipi bora kwa mteja na siyo kufuata sheria kama ilivyo hata kama inamuumiza mteja.
 41. Unapaswa kuwa na mpango wa maisha kabla ya kuweka mpango wa biashara. Biashara siyo kitu pekee na kikuu kwenye maisha yako, bali ni sehemu ya kukufikisha kwenye kitu pekee na kikuu kwenye maisha yako. Kuweka mipango ya biashara kabla ya kuwa na mipango ya maisha ni kuchagua kuyaharibu maisha yako.
 42. Wakati unajaribu kwenda hatua ya juu zaidi kwenye mauzo, usifikiri unajua kila kilichoiwezesha biashara yako kufanikiwa awali. Kuna sababu nyingi zinachangia biashara kufanikiwa, ni vigumu kuzijua zote, hivyo usijiamini kwa sababu moja au chache, unaweza kushindwa vibaya baadaye.
 43. Kuikuza biashara yako zaidi ni swala la wewe kuchagua. Kabla hujakimbilia kukuza zaidi biashara yako jua kwa nini unataka kufanya hivyo. Ukuaji wa biashara unakuja na gharama zake, hakikisha unazijua kabla ya kuingia kwenye hali hiyo.
 44. Kubwa siyo bora mara zote. Mara nyingi biashara ndogo zina nguvu kubwa ya ushindani kuliko biashara kubwa. Mfano biashara ndogo inaweza kubadilika haraka kuliko biashara kubwa. Hivyo usikimbilie kukua kama hujawa tayari.
 45. Kumbuka mahusiano ya biashara hayapaswi kupelekwa kuwa mahusiano binafsi, hasa mahusiano yako na wafanyakazi wako. Yanapaswa kubaki kuwa mahusiano ya kibiashara na msiingie kwenye mahusiano mengine ya karibu, kama ya kirafiki au kimapenzi. Mahusiano yoyote unayotengeneza na wafanyakazi wako nje ya mahusiano ya kibiashara, yanakuja kukugharimu sana wewe.
 46. Kama unapenda kufanya kile ambacho kinafanyika kwenye biashara yako, mfano kuuza, badala ya kupenda kuiongoza biashara, jua unaweza kufanya hicho unachopenda na kuajiri watu wengine waongoze biashara hiyo. Usikwame kukua kwenye biashara yako kwa sababu hupendi kuongoza timu kubwa, kama fursa ipo, wape wanaoweza kuifanya wakusaidie.
 47. Kama umegundua kuna wafanyakazi wanakuibia kwenye biashara yako, dawa siyo kusema wafanyakazi wote hawaaminiki. Bali jua kwamba kuna udhaifu kwenye mfumo wako wa biashara, hivyo rekebisha udhaifu huo. Kama kuna mwanya wa kuiba, hata asiye mwizi anapata ushawishi wa kuiba. Hivyo kama kuna wafanyakazi wanaiba kwenye biashara yako, jua wewe ndiyo unawapa mwanya wa kufanya hivyo.
 48. Unapofika wakati wa wewe kukaa pembeni kwenye uongozi wa biashara yako na kumpata meneja wa kuisimamia kwa karibu, pata mtu unayemwamini kwamba anaweza kufanya maamuzi sahihi na kuyasimamia na kisha wewe angalia ni mchango gani utakaotoa kwenye biashara yako. Siyo mara zote utakubaliana na maamuzi yake, lakini kama ni mtu unayemwamini, utampa nafasi ya kufanya kile anachofikiri ni sahihi.
 49. Utamaduni wa biashara yako ndiyo kiungo muhimu katika kuwapata na kuwatunza wafanyakazi bora kwenye biashara hiyo. usikose fursa ya kutengeneza na kuboresha utamaduni wa biashara yako.
 50. Kazi moja ya biashara yako ambayo huwezi kumpa mtu mwingine kuifanya ni kutengeneza utamaduni wa biashara yako. Hiki ni kitu unachopaswa kukifanya wewe mwenyewe, kwa sababu wew endye mwenye maono makubwa ya biashara yako.
 51. Gharama huwa zina tabia ya kukua kadiri kipato kinavyoongezeka. Unapoanzia biashara chini huwa unakuwa bahili, lakini biashara inapokuwa gharama zinaanza kukua kidogo kidogo na unakuja kustuka mauzo ni makubwa, faida ghafi ni kubwa lakini biashara haitengenezi faida halisi. Ili kudhibiti ukuaji wa gharama, unapaswa kumhusisha kila mtu kwenye biashara.
 52. Angalia na tumia fursa mbalimbali kutuma ujumbe kwa wafanyakazi wako kwamba unajali kuhusu wao ili nao wajali kuhusu biashara yako na kukazana kupunguza gharama pale inapowezekana. Wafanyakazi wako wanazijua njia nyingi za kupunguza gharama kwenye biashara yako.
 53. Watu wako wa mauzo ndiyo wanakuwakilisha wewe kwenye soko lako. Hakikisha unachagua watu wa mauzo ambao watakuwakilisha vyema kwenye soko, wanaoendana na viwango vya biashara yako.
 54. Kuwa makini na watu wa mauzo ambao wana mafanikio makubwa kwenye kuuza na wale ambao wana mpango wa kuja kujiajiri wenyewe. Hawa ni majanga kama ukiwaajiri kwenye biashara yako. Wale ambao ni wauzaji wazuri, huwa wanakazana kuuza na siyo kuangalia mauzo bora. Wale ambao wana mpango wa kuja kujiajiri kuna siku watakuacha, hivyo unakuwa umetumia nguvu nyingi kuwafundisha na wanakuacha. Ajiri watu wa mauzo wa kawaida na kisha wafundishe wewe mwenyewe mbinu bora za mauzo na wazifanyie kazi.
 55. Kuwalipa watu wa mauzo kwa kamisheni kunaweza kutengeneza madaraja kwenye biashara yako na kuondoa ile dhana ya biashara kuendeshwa kama timu inayoshirikiana. Njia bora ya kuwalipa watu kwenye biashara yako, hasa wale wa mauzo ni kuwa na mshahara halafu bonasi ya mwisho wa mwaka pale timu nzima inapovuka lengo na siyo mtu mmoja mmoja. Bonasi inaleta hali ya kufanya kazi pamoja kama timu.
 56. Wafanyakazi wako wote wana mchango kwenye mauzo, kwa namna moja au nyingine. Hivyo mafunzo ya mauzo yanapaswa kutolewa kwa kila mfanyakazi wa biashara yako.
 57. Unapokutana na tatizo linalokukwamisha, omba ushauri kwa watu walio nje. Ni rahisi kwa mtu wa nje kuona tatizo na suluhisho lililo wazi kuliko wewe ambaye tatizo linakuwa limekushika kihisia. Kuwa tayari kupokea ushauri na kuuchuja kulingana na kile unachopitia.
 58. Usichukue ushauri wa biashara kutoka kwa wahasibu. Hawa ni wazuri kwenye kuandaa namba za biashara na hata kueleza historia ya nyuma ya biashara kupitia namba, kwamba nini kilitokea. Lakini kwenye kufanya makadirio ya mbele ya biashara, ni wabovu sana, huwa wanafanya makadirio makubwa ambao hayaendani na uhalisia. Unapotaka ushauri wa biashara, omba kwa mfanyabiashara mwenye uzoefu.
 59. Usichukue ushauri wa biashara kutoka kwa wanasheria. Kazi ya wanasheria ni kukusaidia kutafsiri sheria na mikataba mbalimbali na kuangalia madhara ya maamuzi yako kwenye sheria na mikataba. Kuhusu ushauri wa biashara, hawawezi kujua ni kipi sahihi au siyo sahihi kwako kufanya. Hivyo wasikilize kwa upande wa sheria pekee, na siyo kwa upande wa biashara. Namba 59 hapo juu imeshakuambia ushauri wa biashara uchukue kutoka kwa nani.
 60. Unaweza kuajiri watu wenye uwezo mkubwa hata kama huwezi kuwalipa malipo makubwa wanayotaka. Unachopaswa kufanya ni kuwapa nafasi ya wao kufurahia kile wanachokifanya.
 61. Kila unapokwenda, kuna masomo mengi na mazuri ya kujifunza kuhusu biashara. Kila unayekutana naye ana kitu cha kukufundisha kuhusu biashara. Kila biashara unayokwenda kupata huduma wewe, kuna kitu cha kujifunza kuhusu biashara yako. Fungua macho yako na kuwa tayari kujifunza na utaziona fursa nyingi za kujifunza.
 62. Kutatua tatizo kunachukua hatua mbili, moja unapaswa kuzuia madhara ya tatizo lililotokea na mbili unapaswa kujua chanzo cha tatizo na kukirekebisha. Wengi huwa wanazuia madhara ya tatizo na kusahau kutatua chanzo, hivyo tatizo linaendelea kujirudia kila mara. Kwa kila tatizo hakikisha unajua chanzo chake na kukitatua.
 63. Maandalizi ni silaha bora kwenye ushindani. Usifanye kitu chochote kwa mazoea, hakikisha unakuwa na maandalizi makubwa kwenye kila unachofanya. Kwa kuwa na maandalizi makubwa hakuna anayeweza kukupita.
 64. Kadiri mtu anavyokusukuma ufanye maamuzi ya haraka, ndivyo unavyopaswa kusisitiza kupata muda zaidi. Ukiona mtu anakulazimisha ufanye maamuzi ya haraka kwa kukuambia huna muda au utaikosa fursa, jua kuna kitu anataka kukutapeli au kukuibia. Chukua muda wako na fanya maamuzi sahihi. Hakuna fursa inayokupita, fursa yoyote sahihi kwako itakuwepo ukiwa tayari.
 65. Kuwa tayari kumbeba mtu mpya wa mauzo kwa angalau mwaka mmoja kabla hajaweza kuuza kwa faida inayoweza kurudisha gharama unazomlipa. Ndiyo maana unapaswa kuchagua watu wa mauzo ambao utakaa nao kwa muda mrefu, kwa sababu mwaka wa kwanza hawazalishi, unakuwa unawekeza kwao.
 66. Kama unataka watu wako wa mauzo wafanye mauzo mazuri, wafundishe waelewe jinsi ambavyo biashara yako inatengeneza fedha. Wakijua hilo, watafanya maamuzi sahihi kwenye mauzo.
 67. Fuatilia namba zako za biashara kwa ukaribu sana, zinapobadilika hakikisha unajua nini kimeleta mabadiliko hayo. Ukifuatilia namba zako kwa karibu, utayaona mabadiliko mapema kabla hayajaleta madhara kwenye biashara yako.
 68. Hamasa ndiyo damu ya uhai wa biashara yako. Jua jinsi ya kutengeneza hamasa kwako mwenyewe na hata kwa wafanyakazi wako ili waweze kuikuza biashara yako zaidi.

Rafiki, haya ndiyo mambo 68 ya kuzingatia ili uweze kuikuza zaidi biashara yako. Yasome, yaelewe na kuyaweka kwenye biashara yako na utaweza kupiga hatua kubwa kwenye biashara.

Usikose #MAKINIKIA ya juma hili ambapo tunakwenda kujifunza umuhimu wa kuwa na mpango wa biashara na jinsi ya kuandaa mpango rahisi kwako. Pia tutajifunza mambo ya kuzingatia ili kujenga mahusiano bora na benki na kuepuka changamoto mbalimbali ambazo wafanyabiashara wengi wamekuwa wanazitengeneza pale wanapochukua mkopo na kuishia kupata hasara.

#3 MAKALA YA JUMA; AMRI KUMI ZA BIASHARA.

Kuna misingi, kuna sheria, halafu kuna amri. Unaposikia amri, ni kitu ambacho kinapaswa kuchukuliwa kama kilivyo, hakuna kukibadili au kukiboresha. Amri ni amri na unapaswa kuichukua na kuifanyia kazi kama ilivyo.

Kwenye kitabu cha STREET SMARTS Norm Brodsky anatushirikisha AMRI KUMI ZA BIASHARA ambazo amejifunza kwa uzoefu wake na wa wengine pia. Amri hizi zinagusa maeneo kumi muhimu ya biashara, ambayo unapaswa kuyazingatia kama unataka kufanikiwa kwenye biashara yako.

Kwenye makala ya juma la 37 tumejifunza amri hizo kumi za biashara na jinsi ya kuzitumia kwenye biashara zetu. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ya juma na kuzijua amri hizo, basi chukua hatua ya kuisoma sasa. Unaweza kusoma makala hiyo hapa; Amri Kumi (10) Za Biashara Ambazo Hupaswi Kuzivunja Kama Unataka Kufanikiwa.

Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku kusoma makala nzuri ambazo zitakupa maarifa sahihi na hamasa ya kupiga hatua ili kufanikiwa zaidi.

#4 TUONGEE PESA; WAKATI SAHIHI WA KUANZA KUOMBA MKOPO BENKI.

Kila biashara huwa ina uhaba wa fedha. Biashara zote huwa zina ukomo wa mtaji, na hivyo kama biashara ikiweza kupata mtaji zaidi inaweza kukua zaidi ya pale ulipo sasa. Hii haijalishi ni biashara kubwa au ndogo, uhaba wa mtaji ni kikwazo kwa kila biashara.

Zipo njia mbalimbali za kupata mkopo wa kukuza zaidi biashara, na moja ambayo ni maarufu na rahisi kutumia kwenye biashara ni kuchukua mkopo benki au taasisi za kifedha. Njia hii ni rahisi kwa sababu benki zinafanya biashara ya kutoa mikopo, hivyo zinapenda sana pale zinapopata biashara ambayo inaweza kuchukua mkopo na kuurejesha.

Pamoja na urahisi wa njia hii, wafanyabiashara wengi wamekuwa wanashindwa kupata mkopo wa kukuza biashara zao benki pale wanapokuwa na uhitaji mkubwa wa kupata mkopo huo. Wengi huishia kulalamika kwamba benki haziwajali wakati wana uhitaji mkubwa. Kama nilivyokudokeza hapo, benki huwa zinapenda uhakika wa fedha wanazotoa kurudi, hivyo kama hakuna kitu cha kuwapa uhakika kutoka kwenye biashara yako, hawawezi kushawishika kukupa mkopo.

Kwenye kitabu cha STREET SMARTS, waandishi wanatuambia biashara nyingi zimekuwa zinakosa mkopo benki kwa sababu wafanyabiashara wamekuwa hawajui wakati sahihi wa kuanza kuomba mkopo benki. Wanasema ukienda kuomba mkopo benki pale ambapo una uhitaji mkubwa, una nafasi kubwa ya kuukosa.

Hivyo wanashauri, wakati sahihi wa kuanza kuomba mkopo benki ni pale ambapo huhitaji mkopo kabisa. Pale ambapo biashara yako inaiendesha vizuri na bado hujafikia hatua ya kutaka kuikuza zaidi. Huu ndiyo wakati ambao waandishi wanatushauri tutengeneze mahusiano mazuri na watu wa benki. Kuwa na watu wa benki unaojuana nao, hasa wale maafisa wanaohusika na mikopo ya kibiashara. Kadiri mahusiano yenu yanavyokuwa bora, ndivyo inavyokuwa rahisi kwao kukuamini na kuhakikisha unapata mkopo pale unapokuwa unahitaji.

Watu wa benki wanapaswa kuwa marafiki wako wa karibu, hasa zile benki unazozitumia kibiashara. Mzunguko wako wa fedha unapaswa kupitia benki ili watu wa benki waweze kujionea jinsi ambavyo biashara inakwenda. Kwa kufanya hivi, inapofika wakati wa kuomba mkopo, inakuwa rahisi kukubaliwa.

Uzuri ni kwamba, ukifanya hivyo, kabla hata hujawafuata watu wa benki kuomba mkopo, wao wataanza kukutafuta wewe na kukuambia unakopesheka. Ila hapo unapaswa kuwa makini, usikimbilie kuchukua mkopo kwa sababu benki imekuambia unakopesheka. Benki inapokuambia unakopesheka inamaanisha kwamba ina uhakika wa kukusanya fedha zake kutoka kwako. Hivyo chukua mkopo pale tu unapokuwa unajua unakwenda kuutumiaje kukuza zaidi biashara yako, ambayo tayari inajiendesha vizuri.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; MAUZO SIYO FAIDA.

“People believe that to be successful, all you have to do is generate sales. In fact, what you need is the right kind of sales. The wrong kind can drive you straight into bankruptcy.” – Norm Brodsky

Wengi wanapoingia kwenye biashara huwa wanafikiri kwamba ili kufanikiwa kwenye biashara basi wanapaswa kuuza zaidi. Ukweli ni kwamba, unachohitaji siyo mauzo mengi, bali mauzo sahihi. Mauzo yasiyo sahihi yanaweza kukuondoa kabisa kwenye biashara.

Mauzo sahihi kwenye biashara yako ni yale ambayo yanakupa faida ghafi kubwa, ambayo ukitoa gharama za kuendesha biashara na kubaki na faida halisi. Mfano umenunua viatu pea kumi kwa shilingi elfu 7 kwa kila pea. Ukauza kwa shilingi elfu 10 kwa kila pea. Gharama zako za kuuza ni elfu 2 kwa kila pea. Hapo umebaki na elfu moja kama faida kwa kila pea.

Mauzo mabaya ni yale ambayo yanaleta faida ghafi kidogo, ambayo ukiondoa gharama za kuendesha biashara, hubaki na faida au unapata hasara kabisa. Kwa mfano huo hapo juu wa viatu, umenunua kwa elfu 7, na kuuza kwa elfu 8, huku gharama za kuendesha biashara ni elfu 2 kwa kila pea. Hapo utauza sana, lakini mwisho wa siku kwa kila pea unayouza, kuna elfu moja unayopoteza.

Sasa kama umewahi kusikia watu wakisema chuma ulete kwenye biashara, ni hicho kitendo cha kukazana kuuza zaidi bila ya kujua kama mauzo hayo yanaleta faida au hasara.

Kazana kutengeneza mauzo sahihi kwenye biashara yako na utaweza kufanikiwa sana.

Rafiki, hizi ndizo TANO ZA JUMA LA 37, nina imani umejifunza mambo mengi sana kuhusu biashara, wajibu wako umebaki kuyaweka kwenye matendo ili biashara unayoifanya iweze kukua na kukupa mafanikio makubwa. Kumbuka biashara siyo ngumu kama zinavyoonekana kwa nje, kama mtu utaifanya kwa misingi sahihi.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili la 37 tunakwenda kujifunza umuhimu wa kuwa na mpango wa biashara na jinsi ya kuandaa mpango rahisi kwako. Pia tutajifunza mambo ya kuzingatia ili kujenga mahusiano bora na benki na kuepuka changamoto mbalimbali ambazo wafanyabiashara wengi wamekuwa wanazitengeneza pale wanapochukua mkopo na kuishia kupata hasara.

Usikose #MAKINIKIA haya kwenye channel yetu ya TANO ZA JUMA iliyopo kwenye mtandao wa TELEGRAM. Kama bado hujajiunga na channel hiyo, maelekezo yako hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu