“Remember that to change your mind and to follow someone’s correction are consistent with a free will. For the action is yours alone—to fulfill its purpose in keeping with your impulse and judgment, and yes, with your intelligence.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 8.16
Usichukulie ni kitu cha kawaida kwako kuiona siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Kwa sababu kuna wengi walitamani sana kuiona lakini hawajapata nafasi kama uliyoipata wewe.
Hivyo ianze siku hii kwa shukrani na nenda kaitumie vizuri kwa kuweka vipaumbele sahihi kwako.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUWA TAYARI KUBADILI MAAMUZI…
Tunajua ya kwamba msimamo ni hitaji muhimu sana kwa mafanikio yetu.
Hivyo ili kuonesha masimamo, tumekuwa tunayasimamia maamuzi ambayo tumeyafanya na kutokuyabadili kabisa.
Ni jambo zuri kusimamia kile ambacho umeamua, lakini kama mambo hayapo kama yalivyokuwa awali wakati unafanya maamuzi, hakuna ubaya wowote kubadili maamuzi hayo.
Labda umepata taarifa ambazo hukuwa nazo wakati unafanya maamuzi.
Labda kuna vitu umekuja kuvijua wakati wa kufanya, ambavyo hukuvijua wakati unaweka mipango yako.
Labda kuna changamoto zimeibuka baada ya kuanza kufanya.
Na labda mapenzi yako binafsi yamebadilika kwenye kile ambacho unataka kwenye maisha.
Zote hizo ni hali mbalimbali zinazoweza kukusukuma kufanya mabadiliko kwenye maamuzi yako.
Unapoona inabidi, fanya mabadiliko ili kupata kilicho bora zaidi.
Kung’ang’ana na maamuzi yako haya pale mambo ya nje yanapobadilika siyo ujanja,
Ujanja ni kuwa tayari kubadili maamuzi yako ili yaendane na hali ya tofauti uliyokutana nayo kwenye kufanya, ambayo haikuwepo wakati unapanga.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa tayari kubadili maamuzi yako pale unapopata taarifa mpya au kujua ambacho hukujua awali. Utayari wa kubadilika ndiyo utakaokuwezesha kupiga hatua zaidi kwenye maisha.
#KuwaTayariKubadilika #MsimamoHaimaanishiUsumbufu #MaraZoteKuwaTayariKujifunza
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1