Sisi wenyewe ni mafundi wazuri wa kujiondoa kwenye nafasi ya kuweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yetu. Yaani kama hufanikiwi, kikwazo cha kwanza ni wewe mwenyewe, kabla ya kuja hivyo vikwazo vingine ambavyo ni rahisi kwako kuvilaumu.

Kwanza huwa tunaanza kuishusha na kuona hatuwezi au hatustahili. Tunaona kwa mazingira yanayotuzunguka na kile tunachofanya, hatuna nafasi ya kuweza kufanya makubwa zaidi. Tunaona wale waliofanya makubwa kuna manufaa fulani wameanza nayo ambayo sisi hatujapata nafasi ya kuwa nayo.

Pili tunaingia kwenye mtego wa kuahirisha mambo. Tunajua kabisa kitu sahihi kufanya ili tupige hatua, lakini hatupo tayari kukifanya, hasa kwa sasa. Hivyo tunajiambia tutafanya kesho au tutafanya wakati mwingine. Lakini hiyo kesho huwa haifiki, na sababu yoyote iliyotufanya tuahirishe leo, kesho inakuwa kubwa zaidi.

Kujizuia wewe usiwe adui wa mafanikio yako mwenyewe, kuna hatua mbili muhimu kuchukua.

Moja ni kujiambia na kuamini ya kwamba unastahili kufanikiwa, licha ya ulikotoka na hali unayopitia sasa, unastahili kabisa kufanikiwa, na ndani yako una uwezo huo. Hakuna wa kukuzuia ila wewe mwenyewe.

Mbili ni kuchagua kuchukua hatua sasa, kila unapopanga kufanya kitu basi kifanye kweli, na pale mawazo ya kuahirisha yanapokujia, jiambie NITAFANYA SASA na anza kufanya. Fanya hata kwa hatua chache sana, ni afadhali kuliko kutokufanya kabisa. Ukiwa mtu wa kufanya, unatengeneza fursa zaidi kwako kufanikiwa.

Unastahili mafanikio. Chukua hatua sasa ili kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha