Upo usemi kwamba kama unataka kujua maji ni nini, basi usimuulize samaki.

Ni usemi ambao unaweza kukushangaza, kwa sababu unajua samaki anaishi kwenye maji kila siku, sasa iweje asifae kuulizwa kuhusu maji? Na hiyo ndiyo sababu kwa nini usimuulize samaki kuhusu maji. Kwa sababu maji ndiyo ulimwengu wa samaki, hajawahi kuishi nje ya maji, hivyo hakuna kitu cha tofauti anachojua kuhusu maji.

Dhana hapa ni kwamba, pale mtu anapokuwa amekizoea kitu na kimekuwa sehemu ya maisha yake, ni vigumu sana kwake kuona mapungufu au madhaifu ya kitu hicho. Kwa sababu hicho ndiyo kitu pekee anachokifahamu yeye.

Hivi ndivyo ilivyo kwenye mazoea, tabia na tamaduni zetu. Kuna vitu ambavyo tunavifanya, ambavyo kwa upande wetu ni kawaida kabisa, lakini kwa watu walio nje wanashangazwa navyo. Kwa mfano kama wewe ni mkristo, mfumo mzima wa imani ya kikristo ni kitu cha kawaida kabisa, lakini anapokuja mtu ambaye siyo mkristo, anaweza kushangaa vitu vingi kwenye imani hiyo.

Jinsi ya kutumia hili;

Moja; kuwa makini kwa wale unaowaomba ushauri, kama mtu unayemuomba ushauri ndiyo kitu pekee anachojua, atakupa ushauri unaoegemea kwenye kitu hicho. Au kama unamwomba ushauri kwenye kitu asichojua, basi ushauri wake utakuwa ni kinyume na kitu hicho.

Mbili; tambua upofu wako ulipo, tambua kwamba kuna mambo ambayo umeshayazoea sana kiasi kwamba kwako ni ya kawaida lakini kwa wengine ni ya kushangaza. Hivyo mtu anapokushangaa kwa kile ambacho umezoea, wewe huishii kushangaa pia, unajua kwa nini anakushangaa.

Na mwisho, usikubali kuwa samaki, mara kwa mara nenda nje ya mazoea yako, fanya vitu ambavyo hujazoea kufanya au kinyume na vile ambavyo umezoea kufanya, jifunze vitu ambavyo vinapingana na kile unachoamini. Lengo ni uweze kuwa na uwanja mpana a kufikiri na kufikia maamuzi sahihi badala ya kuwa na mtazamo mwembamba kwenye eneo moja tu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha