“Being unexpected adds to the weight of a disaster, and being a surprise has never failed to increase a person’s pain. For that reason, nothing should ever be unexpected by us. Our minds should be sent out in advance to all things and we shouldn’t just consider the normal course of things, but what could actually happen. For is there anything in life that Fortune won’t knock off its high horse if it pleases her?”
—SENECA, MORAL LETTERS, 91.3a–4

Nani aliyeiona siku hii mpya ya leo na awezaye kusema ni kwa akili na nguvu zake mwenyewe?
Kama yupo basi ni mpumbavu, kwa sababu kuiona siku hii ni bahati ya kipekee sana kwetu.
Kushukuru kwa bahati hii ni kwenda kuitendea vyema siku hii, kutokupoteza muda kwenye mambo yasiyo ya msingi.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari INAWEZA KUTOKEA KWAKO PIA…
Kuna jambo moja la kushangaza kwa sisi wanadamu,
Jambo gumu na baya linapotokea kwa wengine, huwa tunakuwa tayari kuwashauri na kuwafariji kwamba wasijali, yatapita, wawe imara au ni mapenzi ya Mungu.
Lakini jambo hilo hilo linapotokea kwetu sisi wenyewe, tunalalamika na kuona kwa nini itokee kwetu!
Inakuwaje tunafikiria yale magumu na mabaya yatatokea kwa wengine ila siyo kwetu?
Iweje tuwe tayari kuwafariji wengine, lakini tushindwe kujifariji wenyewe?

Ukweli tunaopaswa kuujua ni kwamba kila ambacho tunaona kinatokea kwa wengine, kinaweza kutokea na kwetu pia.
Unapoona wengine wanafiwa na wazazi wao na hilo bado halijatokea kwako, wakati unawafariji jua na hilo linaweza kutokea kwako pia.
Unaoona wengine wanafiwa na watoto wao na hilo halijawahi kutokea kwako, jua linaweza kutokea pia.
Unapoona wengine wanafukuzwa kazi au biashara zao kufa, jua inaweza kutokea kwako pia.
Unapoona mahusiano ya wengine yanavunjika, jua hilo linaweza kutokea kwako pia.
Unapoona wengine wanapata magonjwa ya ajabu na yasiyotibika, jua hilo linaweza kutokea kwako pia.

Kwa kujua kila kinachotokea kwa wengine kinaweza kutokea na kwako, inakuandaa kwa mambo mawili;
Moja ni kuangalia sababu ya kilichopelekea yatokee kwa wengine na kuona kama unaweza kukinga yasitokee kwako.
Mbili ni kujiandaa na kuwa tayari kuyapokea pale yanapotokea.

Kama kitu chochote kinatokea kwenye maisha yako halafu kinakushangaza, yaani hukutegemea kitokee, basi jua umekuwa hujiandai vyema na maisha, umekuwa unaendesha maisha yako kwa kubahatisha.
Kama unajiandaa vyema na maisha kila siku, hakuna kitakachotokea kikakushangaza, maana unajua chochote kinaweza kutokea kwako.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujiandaa na kujua chochote tunachoona kinatokea kwa wengine, kinaweza kutokea na kwako pia.
#TegemeaUsiyotarajia #MipangoSiyoMatumizi #DuniaHaiendiUnavyopangaWewe

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1