Mtu mmoja amewahi kuniambia maneno mabaya, siku inayofuata akaniomba msamaha kwa maneno hayo mabaya aliyoniambia, akisema siyo yeye bali pombe ndiyo zilimfanya atoke maneno hayo. Nilimsamehe lakini nikamwambia kitu kimoja, pombe haiongezi maneno kwenye akili yako, bali inaondoa ile aibu ya wewe kuyatamka, hivyo fikra hizi zilikuwepo, lakini bila ya pombe hukuwa unathubutu kuzieleza wazi.

Hivi pia ndivyo ilivyo kwenye kazi au biashara tunazofanya. Yale matokeo unayozalisha kwenye kazi au biashara unayofanya, ni kiashiria cha kile kilicho ndani yako. Hivyo kama unataka kumpima mtu na kujua nini kipo ndani yake, angalia matokeo anayozalisha kwenye kazi au biashara anayofanya.

Kama mtu anafanya kazi ya hovyo na isiyo na viwango vizuri, ni kwa sababu mtu huyo ndani yuko hovyo na hana viwango vyovyote alivyojiwekea. Hivyo anachozalisha kwenye kazi au biashara ni kiashiria cha kilichopo ndani yake.

Kama mtu anachelewa kwenye kazi au biashara yake, kama anashindwa kumaliza kazi zake kwa wakati, ni kwa sababu ndani yake ana uchelewaji.

Kama mtu amechoshwa na kazi au biashara anayoifanya, ni kwa sababu ndani yake amechoshwa na yeye mwenyewe.

Kama mtu hapendi kile anachofanya, ni kwa sababu ndani yake hajipendi yeye mwenyewe.

Kwa kujua hili, unapaswa kuanza kuchukua hatua ndani yako kabla hujachukua hatua za nje ili kuboresha kazi au biashara yako.

Tengeneza kwanza taswira mpya ya ndani yako, anza kujiona ni mtu bora, mtu ambaye anazalisha matokeo bora na hapo utaweza kuzalisha matokeo mazuri kwenye kazi au biashara yako.

Matokeo mazuri kwenye kazi au biashara unayofanya yanaanzia kwenye taswira yako ya ndani, jinsi unavyojichukulia wewe mwenyewe. Anza kutengeneza taswira hii na utaweza kupiga hatua kubwa kwenye kile unachofanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha