Sina fedha ya kumudu kitu hicho na sina muda wa kufanya kitu hicho ni visingizio viwili ambavyo karibu kila mtu amekuwa anavitumia kwenye baadhi ya mambo anayofanya.
Tumekuwa tunaona kama hivi ndiyo vikwazo kwetu kupiga hatua zaidi kwenye maisha, kwamba kama tusingekuwa na ukomo wa fedha au muda, basi tungeweza kufanya chochote tunachotaka.
Tunachopaswa kujua ni kwamba, kila mtu ama ukomo wa vitu hivi viwili, haijalishi ana muda au fedha kiasi gani, kuna wakati anafikia ukomo wake.
Hivyo kutumia vitu hivi viwili kama sababu ya kushindwa kupiga hatua siyo sahihi. Kwa sababu tumewaona wengi wakipiga hatua licha ya kuwa na ukomo mkubwa kwenye maeneo hayo mawili.
Ndiyo maana leo nakuambia kinachowakwamisha wengi siyo fedha au muda, bali vipaumbele ambavyo mtu unakuwa umejiwekea kwenye fedha na muda.
Unapojiwekea vipaumbele sahihi na muda au kipato kidogo ulichonacho ukaelekeza kwenye vipaumbele hivyo, unaweza kupiga hatua kubwa zaidi.
Lakini kama una muda na fedha kidogo na huna kipaumbele chochote unachofanyia kazi, muda na fedha haviwezi kukutosha kamwe. Kwa sababu usipokuwa umeupangilia muda, unajikuta una mengi ya kufanya na huna muda wowote wa ziada. Usipopangilia fedha, kila unapoipata yanaibuka matumizi ambayo hata hayakuwepo, hivyo unajikuta kila wakati fedha hazitoshi.
Acha mara moja kutumia ukomo wa muda na fedha kama kikwazo na anza kuangalia vipaumbele ulivyonavyo. Angalia muda mchache ulionao sasa unaupeleka kwenye mambo yapi muhimu. Pia angalia kiasi kidogo cha fedha unachopata sasa unakitumia kufanya nini.
Ni jambo la kushangaza pale mtu anapolalamika hana muda, lakini mtu huyo huyo yupo kwenye mitandao ya kijamii, anafuatilia kila habari, na hakosekani kwenye kila aina ya ubishi kuhusu siasa, michezo na mambo mengine yanayoendelea. Huyu siyo kwamba hana muda, bali hana mpangilio mzuri wa muda alionao.
Ni jambo la kushangaza pale mtu anapolalamika kipato chake ni kidogo, lakini mtu huyo huyo ananunua vitu vya anasa, kama vilevi, anachangia kila aina ya sherehe anayoombwa mchango na kununua kila aina mpya ya nguo inayotoka. Kama mtu huyu angeweka vipaumbele sahihi kwenye kipato chake kidogo, angeweza kupiga hatua zaidi.
Hujakosa muda wala fedha, bali umekosa vipaumbele sahihi kwenye muda na fedha. Anza kufanyia kazi vipaumbele vyako sasa na utaweza kuwa na matumizi sahihi ya muda na fedha kidogo ulizonazo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,