“How appropriate that the gods put under our control only the most powerful ability that governs all the rest—the ability to make the right use of external appearances—and that they didn’t put anything else under our control. Was this simply because they weren’t willing to give us more? I think if it had been possible they would have given us more, but it was impossible.
—EPICTETUS, DISCOURSES, 1.1.7–8
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii mpya na bora sana kwetu.
Tumeipata nafasi nyingine nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UTHAIFU UNAPOKUWA UIMARA…
Kati ya mvua na jua bora nini?
Kama umelima mazao yako na yako kwenye hatua ya ukuaji ambapo yanahitaji maji kwa wingi, mvua ni bora kwako.
Lakini kama unafanya ujenzi mjubwa ambao unahitaji kuweka zege eneo kubwa, jua ni bora kwako.
Sasa pata picha kana ingekuwa ndani ya uwezo wetu sisi binadamu kuamua kama sasa inyeshe mvua au liwake jua!
Hebu pata picha ingekuwaje yani.
Wewe unataka jua, na jirani yako anayaka mvua, na wote mna uwezo sawa wa kuita kile mnachotaka.
Tungejikuta tunatumia muda mwingi kubishana nani anastahili kupata kile anachotaka, yaani mvua au jua.
Tungechukiana pale ambapo mtu anapata haki ya kuwasha jua wakati sisi tulitaka mvua.
Lakini kwa swala la mvua kuwa nje ya uwezo wetu, halitusumbui, likiwaka jua tunalitumia vizuri, ikinyesha mvua nayo pia tunaitumia vizuri.
Unaweza kuona udhibiti huu wa mvua au jua kuwa nje ya uwezo wetu ni udhaifu, lakini kwa hakika ni uimara. Inatupa utulivu na kutuwezesha kuchukua hatua sahihi badala ya kusuguana na wengine juu ya maamuzi ya nani ni sahihi.
Kadhalika kwenye kuwabadili au kuwadhibiti wengine.
Kuna wakati unatamani ungeweza kuwadhibiti wengine na kuwabadili wawe kama unavyotaka wewe. Lakini hilo linashindikana kwa sababu udhibiti wa wengine upo nje ya uwezo wetu.
Sasa kabla hujafikiria huo ni udhaifu, hebu jiulize kama ingekuwa ndani ya uwezo wa binadamu kuwadhibiti na kuwabadili wengine, leo hii ungekuwa wapi?
Fikiria jinsi wazazi wako walikuwa wanajaribu kukudhibiti,
Walimu nao wakajaribu kukudhibiti,
Watu wa karibu, mwenza, mwajiri na kadhalika.
Kama hawa wote wangefanikiwa unafikiri ungebaki kuwa mtu?
Ungeishia kuwa kana kinyago cha watu wengine.
Hivyo kushindwa kuwadhibiti na kuwabadili, siyo udhaifu kwetu, bali ni uimara kwa sababu inatufanya tuwe huru kuchagua kuyaishi maisha yetu.
Kila kitu unachokiona kana udhaifu kwenye maisha yako, hapo ndipo penye uimara mkubwa sana kwako. Ujue nw utumie vizuri.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutumia kila udhaifu kama uimara wako na kupiga hatua zaidi.
#UdhaifuNdiyoUimara #HangaikaNaYaliyoNdaniYaUwezoWako #UsisumbukeNaYaliyoNjeYaUwezoWako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1