Mpendwa rafiki yangu,

Mtazamo ulionao juu ya ndoa yako na jinsi unavyomchukulia mwenzako ndiyo matokeo halisi unayopata sasa. Jinsi tunavyokuwa tunawachukulia wenzetu, asili nayo inatupa matokeo ya kile kile tunachofikiria.

Gia uliyoingia nayo kwenye ndoa ndiyo iliyokufikisha hapo ulipo sasa, ukiingia kwenye ndoa kwa gia nzuri yaani kwa mtazamo sahihi basi utakuwa unapata matokeo ya chanya na sahihi.

Kile ambacho tunakiwaza sana katika ndoa zetu ndiyo kinachotokea hivyo kama unawaza mambo  chanya basi yatakuja kwenye ndoa yako.

Waswahili wanasema kuwa, ukiona vyaelea ujue vimeundwa hivyo ukiona ndoa bora yoyote ujue kuna siri ya ushindi nyuma yake. Ndoa yoyote bora ina kitu cha kipekee kimoja ambacho kila mtu anaalikwa kujifunza na siyo kingine bali ni uvumilivu.

Uvumilivu unawasaidia wanandoa kuchukuliana kwa sababu kila mmoja wetu ana tabia zake kwa mfano, mke au mume wako uliye naye ana mazuri na mapungufu yake hivyo huwezi kumpata mtu ambaye hana mapungufu.

Kama uliye naye ulimpenda kwa mazuri basi tambua kuwa ana mapungufu yake ili sasa muweze kuishi kadiri ya mapungufu ndiyo mntakiwa kuvumiliana na kuchukuliana. Bila hivyo maisha ya ndoa yanakuwa ni magumu sana.

Wanandoa wanatakiwa kuvumiliana, kutaka mke au mume awe kama wewe ni kujiandaa kushindwa kwa sababu hatuwezi kuwa sawa, kila mtu ana udhaifu wake. Ni kitu ambacho hakiwezekani hata siku moja.

Raisi mmoja wa marekani aliwahi kusema ukitaka ubaya kwa mtu tegemea kuupata, kumbe basi kama tunategemea mazuri kutoka kwa mtu tutayapata.

SOMA; Hii Ndiyo Dalili Ya Ndoa Isiyokuwa Na Uhai

Na kila mtu ana mabaya yake, sasa kwani wewe mabaya ndiyo shabaha yako? hapana hivyo basi kila mtu aangalie mazuri anayoyanufaika nayo kutoka kwa mwenzake na achana nayo kwa sababu kila mtu ana udhaifu wake hivyo jiandae tu kuchukua mazuri na mengine mnatakiwa kuchukuliana.

Uvumilivu katika upendo ndiyo ndoa yenyewe, bila kuvumiliana hakuna ndoa yoyote inaweza kufika mbali na kuwa bora hata siku moja.

Hatua ya kuchukua leo; jifunze kumvumilia mwenzako wa ndoa, kama ulimpenda kwa mazuri basi jua naye ana udhaifu wake, hivyo msaidie pale anapokuwa kwenye ule udhaifu ambao unaona anaenda ndivyo sivyo.

Kwahiyo, maisha ya ndoa ni maisha ya umoja, wanandoa wanatakiwa kupendana na kunyenyekeana, pasipo unyenyekevu ndoa inakuwa ni ya kibabe, palipo na unyenyekevu, upendo , amani, uvumilivu, furaha hukaa ndani yake.

Makala hii imeandikwa na

Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa  http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com //kessydeoblog@gmail.com

Asante sana