“But the wise person can lose nothing. Such a person has everything stored up for themselves, leaving nothing to Fortune, their own goods are held firm, bound in virtue, which requires nothing from chance, and therefore can’t be either increased or diminished.”
—SENECA, ON THE FIRMNESS OF THE WISE, 5.4

AMKA mwanamafanikio,
Siyo tu uamke kutoka usingizini, bali pia uamke kutoka kwenye mazoea ambayo umekuwa nayo kila siku.
Ichukue siku hii mpya na chagua kuiishi kwa upya, kwa kwenda kuchukua hatua kubwa na za tofauti.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UWEKEZAJI BORA KABISA UNAOWEZA KUFANYA…
Kuna uwekezaji wa aina nyingi unaoweza kufanya,
Unaweza kuwekeza kwenye kazi na biashara yako, na hapo ukaongeza zaidi kipato chako.
Unaweza kuwekeza kwenye mali mbalimbali na hapo ukajitengenezea uhuru wa kipato.
Unaweza kuwekeza kwenye masoko ya mitaji na hapo ukaingiza kipato bila ya kufanya kazi.

Lakini aina zote hizo za uwekezaji siyo salama,
Unaweza kupoteza kazi na biashara yako muda wowote na ukabaki huna cha kufanya.
Unaweza kupoteza mali zako zote, kupitia ajali na majanga mbalimbali au hata kutaifishwa na serikali.
Unaweza kupoteza uwekezaji uliofanya kwenye masoko ya mitaji pale uchumi unapoyumba.

Upo uwekezaji mmoja ambao ni bora sana kwako, uwekezaji ambao huwezi kuupoteza kwa namna yoyote ile, hata kitokee kitu gani, uwekezaji huo utabaki kuwa kwako na utakusaidia kufanya maamuzi bora.
Uwekezaji huo ni kuwekeza ndani yako mwenyewe,
Na hapa unalenga vitu viwili;
Moja; kuwa na hekima
Mbili; kuwa na tabia njema.

Ukifanya uwekezaji ndani yako kwa kusimamia maeneo hayo mawili, ukawa na hekima na tabia njema, kwa hakika hakuna kitakachoweza kukuteteresha kwenye haya maisha.
Utakutana na magumu na changamoto, lakini hekima itakuwezesha kuyavuka.
Utaweza kupoteza kila ulichonacho sasa, lakini tabia njema itakupa fursa ya kuanzia popote na kurudi tena kwenye kilele.

Haimaanishi kwamba hupaswi kuwekeza kwenye maeneo hayo mengine, bali usisahau kufanya uwekezaji huu ambao ndiyo muhimu zaidi kwako, ambao utawezesha uwekezaji mwingine unaofanya uwe bora zaidi.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufanya uwekezaji ndani yako, kwa kuongeza hekima yako na kuwa na tabia njema.
#WekezaNdaniYako #JijengeeHekima #KuwaNaTabiaNjema

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1