Kila mtu kuna gharama lazima alipe kwenye maisha yake, hakuna anayeweza kukwepa hilo.

Ambacho mtu anaweza kuchagua ni kulipa keshi au mkopo, yaani kulipa sasa au kulipa baadaye, lakini hakuna anayeweza kukwepa kulipa.

Kulipa keshi ni pale unapochagua kuikabili gharama unayopaswa kulipa sasa, kuweka kazi na juhudi sasa ili kupata matokeo mazuri baadaye.

Kulipa kwa mkopo ni pale unapochagua kuisogeza mbele gharama unayopaswa kulipa, kuikwepa kwa sasa na kuamini baadaye ndiyo utaweza kuikabili au kuikwepa. Kwa sababu huwezi kuikwepa, unaishia kukutana nayo baadaye, tena ikiwa kubwa kuliko sasa.

Unaweza kuteseka sasa na maisha lakini ukajenga maisha mazuri ya baadaye ambayo hayatakuwa na mateso tena. Au unaweza kuepuka kujitesa sasa, lakini ukawa umetengeneza mateso makubwa ya baadaye.

Mfano, ukiwa kwenye ajira, unaweza kuwa kama waajiriwa wengine, usijitese kwa namna yoyote ile na ukaona maisha yako ni mazuri, lakini kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo ajira hiyo inakufanya mtumwa na usiwe na uhuru kabisa.

Au unaweza kujitesa ukiwa kwenye ajira yako, kwa kuanza biashara yako ya pembeni, kuweka juhudi kubwa katika kuikuza na baadaye biashara hiyo ikakupa uhuru mkubwa wa kuweza kuacha ajira yako.

Tofauti hapo ni kuchagua, unachagua kulipa keshi au mkopo. Kumbuka kila mtu ataumia na kuteseka kwenye haya maisha, swala ni unachagua kuumia na kuteseka lini, sasa au siku zijazo.

Kila mara unapokwepa maumivu na mateso, jiulize kama kweli upo tayari kukabiliana na vitu hivyo baadaye.

Maamuzi mazuri ni kukabiliana na chochote sasa, kwa sababu hujui kesho itakuwaje.

Lipa keshi mara zote, inapokuja kwenye kazi, juhudi na kujituma ili kufanikiwa zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha