“Better to trip with the feet than with the tongue.”
—ZENO,
Ni siku nyingine mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KIUONGO UNACHOPASWA KUWA NACHO MAKINI..
Ni ulimi wako,
Teleza kwa miguu, lakini usiteleze kwa ulimi.
Kwa sababu ukianguka unaweza kuinuka na kuendelea na yako,
Lakini ukishatoa neno, huwezi kulirudisha tena, huwezi kubadili madhara yake, hasa pale neno hilo linapokuwa baya na linaloumiza.
Chunga sana ulimi wako, ni rahisi kusema lakini madhara ya unachosema yanaweza kuwa makubwa sana na yakawa kikwazo kikubwa kwako baadaye.
Neno likishakutoka huwezi tena kulirudisha.
Ukishasema kitu, huwezi tena kukifuta.
Maana watu wanakuwa wameshasikia na kutafsiri wawezavyo wao wenyewe.
Kabla hujasema neno lolote, tafakari mara mbili madhara yake,
Na kama huna uhakika, ni bora kukaa kimya.
Wanasema mpumbavu akikaa kimya anaweza kudhaniwa ni mwerevu.
Na ni bora watu wakudhanie ni mjinga kwa kukaa kimya, kuliko kuropoka na ukaweka wazi na kuthibitisha kabisa.
Kwa zama tunazoishi pia, vidole vyako unapaswa kuwa navyo makini sana, hasa unapokuwa kwenye mitandao ya kijamii au mawasiliano mengine.
Unaweza kuandika kitu na kikaleta madhara makubwa sana.
Japo unajiambia unaweza kufuta ulichoandika, ukishaweka kitu mtandaoni, hata kama utafuta, mtandao huwa hausahau, kitaendelea kuwepo na kuna wengine wanaweza kukitunza vizuri kwa ajili ya ushahidi wa baadaye.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa makini na ulimi wako na vidole vyako pia. Siku ya kutafakari kwa umakini kabla ya kusema au kuandika chochote.
#DhibitiUlimiWako #DhibitiVidoleVyako #TafakatiKablaYaKusemaAuKuandika
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1