“It’s in keeping with Nature to show our friends affection and to celebrate their advancement, as if it were our very own. For if we don’t do this, virtue, which is strengthened only by exercising our perceptions, will no longer endure in us.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 109.15

Ni jambo la kushukuru sana sisi kuweza kuiona siku hii mpya ya leo,
Hakuna hata mmoja wetu awezaye kusema ameiona siku hii kwa akili na nguvu zake mwenyewe,
Bali ni jambo la bahati kuiona siku hii, na hivyo tunapaswa kuitumia vizuri sana, kwani hatutakuja kupata siku nyingine kama hii.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari FURAHIA MAFANIKIO YA WENGINE…
Kwa asili ni vigumu sana kwetu sisi binadamu kufurahia mafanikio ya wengine, hasa pale ambapo sisi tunakuwa jatujafikia ngazi hizo ambazo wengine wamefikia.
Kuna hali fulani ya wivu huwa inatuingia pale tunapoona wengine wanapiga hatua kuliko sisi.
Huwa tunafikiri kupata kwao basi ni kukosa kwetu, kama vile kuna uhaba wa mafanikio.
Lakini hilo siyo sahihi, hakuna uhaba wa mafanikio na kufanikiwa kwa mwingine hakuzuii kufanikiwa kwako.

Tunapaswa kufurahia na kushangilia mafanikio ya watu wengine kama vile ni mafanikio yetu. Hii ni kwa sababu;
👉🏼Kufanikiwa kwa wengine ni kiashiria kwamba walichofanya kinawezekana, hivyo hata sisi tunaweza kufika kule walikofika wao kama tutachukua hatua sahihi.
👉🏼Unapofurahia mafanikio ya wengine unakuwa tayari kujifunza kupitia wao na hivyo unakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa. Wale wanaochukia au kukosoa mafanikio ya wengine, huwa wanajifunga wao wasifanikiwe.
👉🏼Unapofurahia mafanikio ya wengine unakuwa umejiweka kwenye mtazamo sahihi unaoendesha asili, mtazamo wa utele na hivyo kuwa tayari kupokea mafanikio yako pia.

Kila ulipo, unapoona kuna mwingine amepiga hatua kubwa, furahia, mpongeze kweli kutoka ndani ya moyo wako na omba kujifunza kutoka kwake.
Achana na akili za walioshindwa, ambao wakiona mtu amefanikiwa badala ya kujifunza kwake wanaanza kuzusha maneno kama; ana bahati, ameiba, ametapeli, ana majini, amesaidiwa na mengine kama hayo.
Unapoona mwingine anapiga hatua, kuna kitu cha tofauti anachofanya.
Ukiyafurahia mafanikio yake, utaweza kujifunza na weae kufanikiwa pia.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufurahia na kusherekea mafanikio ya wengine, kisha kujifunza ili na wewe ufanikiwe pia.
#DuniaInaUtele #KufanikiwaKwaWengineNiKufanikiwaKwako #JifunzeKwaWaliofanikiwa

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1