“Yes, getting your wish would have been so nice. But isn’t that exactly why pleasure trips us up? Instead, see if these things might be even nicer—a great soul, freedom, honesty, kindness, saintliness. For there is nothing so pleasing as wisdom itself, when you consider how sure-footed and effortless the works of understanding and knowledge are.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 5.9

Hongera sana mwanamafanikio kwa nafasi hii nyingine nzuri tuliyoiona leo.
Ni bahati sana kwetu kuiona siku hii,
Hivyo tunapaswa kuitumia vyema, kwa kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari RAHA ILIYO JUU…
Kuna vitu mbalimbali ambavyo huwa tunavifanya na vinatupa raha, lakini raha hizo tunazozipata huwa hazidumu kwa muda mrefu.
Kutumia kilevi kunakupa raha, lakini raha hiyo hupotea baada ya ulevi kuisha mwilini.
Kufanya mapenzi kunakupa raha, lakini baada ya muda mfupi raha hiyo inaisha.
Kufikia lengo fulani ulilojiwekea kunakupa raha, lakini ghafla unaona kuna malengo mengine makubwa zaidi unayopaswa kufikia, na hapo raha ya mwanzo inaisha.

Tumekuwa tunatamani raha hizo tunazopata zidumu,
Na hilo limetufanya kuwa watumwa wa vitu hivyo vinavyotupa raha,
Mwishowe tunaishi maisha ya kukimbiza raha kama kipepeo vile, kila tukiikamata inatuponyoka, inabidi tuikimbize tena.

Lakini Marcus Aurelius anatuambia ipo raha moja iliyo juu, raha ambayo haiishi, raha ambayo haina utegemezi na raha ambayo huna haja ya kuikimbiza.
Raha hiyo ni ile inayotokana na tabia njema ambazo ni HEKIMA, UJASIRI, HAKI na KIASI.
Kwa kujijengea tabia hizo, kila wakati unakuwa na raha inayodumu na hakuna chochote kinachoweza kukuyumbisha.
Raha iliyo juu inaanzia ndani yako, kwa tabia ambazo unakuwa umejijengea.
Kama raha haianzii ndani yako, raha yoyote ya nje itakusumbua na kukufanya kuwa mtumwa zaidi kwa kuendelea kuitegemea huku ikiwa haitegemeki.

Jijengee tabia njema na ziishi kila siku na maisha yako yatakuwa ya raha idumuyo.
Ni kitu gani kitakusumbua pale unapokuwa na hekima ya kufanya maamuzi sahihi mara zote?
Ni kitu gani kitakutisha pale unapokuwa tayari kukabiliana na chochote kinachoweza kutokea.
Nini kitakusumbua pale unaposimamia haki na usawa kwenye mambo yote na kwa kila anayekuzunguka?
Ni nani anaweza kukutumikisha ikiwa una kiasi kwenye kila unachofanya na unaweza kujidhibiti wewe mwenyewe?
Ni raha iliyo juu na isiyoshindwa pale unapojijengea tabia hizo njema.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujijengea tabia zilizo njema ili kuweza kuwa na raha idumuyo milele.
#RahaInaanziaNdani #TabiaNjemaZinalipa #UsiweMtumwaWaMamboYaNje

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1