“How rotten and fraudulent when people say they intend to ‘give it to you straight.’ What are you up to, dear friend? It shouldn’t need your announcement, but be readily seen, as if written on your forehead, heard in the ring of your voice, a flash in your eyes—just as the beloved sees it all in the lover’s glance. In short, the straightforward and good person should be like a smelly goat—you know when they are in the room with you.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 11.15
Ni bahati iliyoje kwangu mimi na wewe rafiki yangu kuiona siku hii nyingine nzuri ya leo.
Ni fursa ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari HUNA HAJA YA KUTANGAZA…
Mtu ameshawahi kukuomba ushauri, na ukaona unachotaka kumwambia kitakwenda kumuumiza, lakini huna budi bali kumwambia. Lakini katika kumwambia ukaanza maelezo yako kwa kusema, “Naomba niwe mkweli kwako…” au “Hapa nakwenda kukupa ukweli mchungu…”
Kutumia maneno kama hayo inaweza kuonekana ni kawaida na kwamba inapunguza maumivu ya ukweli unaokwenda kuutoa.
Lakini tukienda kwa ndani zaidi hilo linamaanisha nini?
Ina maana wakati huo uliotangaza kusema ukweli ndiyo wakati pekee unasema ukweli, wakati mwingine wote huwa husemi ukweli?
Rafiki, kama wewe ni msemaji wa ukweli, huna haja ya kutangaza hilo, mpaka mtu anakuja kwako, anapaswa kujua kwamba kila neno linalotoka kwenye kinywa chako ni ukweli.
Ipanaswa kujulikana na kila anayekuzunguka na hivyo haina haja ya kutangaza kila mara.
Kama ambavyo huna haja ya kutangaza jinsia yako kwa watu wako wa karibu (si wote wanaijua?) Ndivyo pia huna haja ya kutangaza kwamba sasa unasema ukweli.
Ukweli unapaswa kuwa msingi wako, kwa kila unachosema na kufanya kusimama kwenye ukweli.
Kila anayekuzunguka anapaswa kujua hilo, na usilivunje.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kusimamia msingi wa ukweli kwenye kila jambo unalofanya na kujulikana hivyo bila hata ya kutangaza.
#UkweliHaufichiki #JulikanaKwaUnavyofanyaSiyoUnavyosema #UsitakeKumfurahishaKilaMtu
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1