Jifunze kujitofautisha wewe na kazi yako, kwa sababu hivyo ni vitu viwili tofauti kabisa. Wewe ni tofauti kabisa na kile unachofanya, japo mna uhusiano wa karibu.
Kuweza kufanya hili, kunakusaidia sana kuwa na maisha tulivu na yasiyoyumbishwa kwa namna yoyote ile.
Kwa mfano pale unapomwelezea mteja kuhusu kile unachofanya kwa lengo la kumshawishi anunue, halafu akakataa kununua, ni rahisi sana kukata tamaa na kuona kwamba wateja wamekukataa wewe. Lakini huo siyo ukweli, mteja hajakukataa wewe, bali amekataa kile unachouza. Huenda hakijamfaa yeye, huenda hakiendani na yeye, lakini siyo kwa sababu wewe una shida yoyote au hufai. Kwa kujua hili inakusaidia kuendelea kuwashawishi wateja wengine. Usipojua hili utakata tamaa na kuona wateja hawakutaki.
Mfano mwingine ni pale unaposhindwa kwenye kitu unachofanya, iwe ni kwenye kazi au biashara, pale unapojaribu kufanya kitu fulani halafu ukashindwa kupata matokeo ambayo ulitegemea kupata. Ni rahisi kujiona hufai na huwezi, lakini hapo ni kama utashindwa kujitofautisha wewe na kile unachofanya. Ukijitofautisha wewe na kile unachofanya, utajua kabisa umeshindwa kwa sababu huna ujuzi au uzoefu sahihi kwenye kitu hicho, na hujashindwa kwa sababu hufai. Hivyo kama utaweka juhudi kwenye kujifunza na kujijengea uzoefu, utaweza kufanya vizuri wakati mwingine.
Kama tulivyoona kwenye mifano hiyo miwili hapo juu, kushindwa kujitofautisha wewe na kile unachofanya ndiyo kinachangia wengi kukata tamaa, hasa pale wanapokataliwa au kushindwa, kwa kuona kwamba wao ndiyo hawafai. Lakini unapoweza kujitofautisha wewe na kile unachofanya, chochote kinachotokea hakikutetereshi, kwa sababu unajua ni matokeo tu na unaweza kuyafanya kuwa bora zaidi wakati mwingine.
Wewe kama nafsi ni kitu kikubwa sana, usijilinganishe na kitu kingine chochote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kwa ujumbe mzuri na hasa wewe kujitofautisha na kile unachofanya. Na pengine kupelekea kukata tamaa.
LikeLike
Ni kweli.
LikeLike
Nitaanza kujitofautisha na kile ninachofanya ili nisikate tamaa. Asante sana kwa ujumbe mzuri.
LikeLike
Karibu sana.
LikeLike