Kabla ya kuja kwa mitandao ya kijamii, ilikuwa rahisi sana kuwaamini watu kwenye kile wanachotuambia. Tumekuwa tunaona mambo kwa nje na kuamini ndani pia mambo ni mazuri kama yanavyoonekana nje.

Lakini ukuaji wa mitandao ya kijamii imefanya tuone kitu cha tofauti kabisa. Watu ambao tunayajua maisha yao kwa uhalisia, wanapoweka picha na mambo yao mtandaoni wanakuwa wa tofauti kabisa. Na wale ambao tumewajua kupitia mtandao, tunapokuja kukutana nao kwenye uhalisia wanakuwa tofauti kabisa na wanavyoonekana mtandaoni.

Ni rahisi kusema mitandao inadanganya, lakini ukweli ni kwamba mitandao hii inatupa ukweli. Na ukweli wenyewe ni kwamba, kila mtu huwa anadanganya kwenye kila kitu. Mitandao ni njia tu ya watu kukamilisha uongo wao na siyo sababu ya wao kudanganya.

Watu wamekuwa wanadanganya mara zote. Watu huwa wanadanganya kuhusu kipato wanachoingiza, kuhusu kiwango chao cha kujiamini, kuhusu kiwango chao cha furaha, kuhusu kiwango cha kazi wanazofanya, kuhusu mambo yanavyokwenda kwa upande wao na mengine mengi.

Karibu kila kitu ambacho watu wanajisifia nacho, wanakuwa wamedanganya au wameongeza chumvi kidogo. Najua unajua jinsi ilivyorahisi watu kuweka picha nzuri mitandaoni lakini zile mbaya hawaziweki.

Watu huwa wanadanganya kwenye mambo mengi wanayojieleza au kujisifia nayo. Na hili linapaswa kukupa funzo kubwa sana, kwamba usijaribu kujilinganisha na mtu yeyote yule. Kwa sababu unapofanya hivyo, unajilinganisha na uongo, hivyo utakuwa unajitesa wewe mwenyewe.

Kuangalia picha za watu mtandaoni ambapo kila wakati wanaweka picha wakiwa wanafurahia na kufanya starehe, ni rahisi kusema wao wana maisha mazuri na wewe una maisha magumu. Lakini unajilinganisha na kipande kidogo sana cha maisha ya mtu, ambapo siyo maisha halisi ya mtu.

Badala ya kujilinganisha na uongo wa wengine, weka mkazo kwenye ukweli wako. Chagua kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi kila siku mpya, jilinganishe na jana yako, jisukume zaidi kila siku mpya na vunja rekodi zako mwenyewe.

Kama unataka maisha ya mateso kwenye hii dunia, basi jaribu kujilinganisha na mtu yeyote yule, utaumia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha