Bahati mbaya sana kwetu sisi binadamu ni kwamba huwa tunajijua kupitia magumu. Pale mambo yanapokuwa mazuri na rahisi huwa tunabweteka na kujisahau, kuona kila kitu kinakwenda vizuri na hatuna haja ya kujisumbua.

Ni pale mambo yanapokwenda tofauti na tulivyozoea ndiyo tunasukumwa kuchukua hatua za tofauti, kufikiri tofauti na hapo ndipo tunapojijua kwa undani.

Huwezi kujijua wewe mwenyewe vizuri kuhusu kazi yako kama hujawahi kukutana na magumu kwenye kazi, kama hujawahi kufukuzwa kazi bila ya kutegemea au kunyanyaswa kwenye kazi kiasi cha kushindwa kuendelea nayo, unakuwa hujajijua vizuri. Tuna mifano mingi sana kwenye hili, unakuta mtu amefanya kazi moja kwa muda mrefu, na kuwa ameshaizoea, linatokea tatizo ambalo linakatisha kazi hiyo na hapo analazimika kufanya kitu cha tofauti, baadaye tatizo hilo linaonekana ni baraka kwake.

Huwezi kujijua wewe mwenyewe vizuri kwenye biashara yako kama hujawahi kukutana na magumu kwenye biashara hiyo. Wakati unaingia kwenye biashara unakuwa na mipango mizuri na matumaini makubwa, kama mambo yatakwenda ulivyopanga unaenda kwa mazoea. Ni mpaka pale unapokutana na changamoto kubwa kama kupata hasara, biashara kufa na mengine mengi ndiyo unajifunza kweli kuhusu biashara na wewe mwenyewe. Katika magumu hayo ndiyo unagundua uliyochagua haikuwa biashara sahihi kwako na hivyo kwenda kwenye biashara sahihi.

Ujumbe muhimu sana wa kuondoka nao leo ni huu; kupitia magumu na changamoto ndiyo tunajijua vizuri sisi wenyewe, ndiyo tunajua nini hasa tunachotaka, ndiyo tunajua uwezo mkubwa uliopo ndani yetu. Hivyo tunapokutana na magumu, tusiyakimbie, badala yake tuyakaribishe kwa sababu yanakuja na manufaa makubwa kwetu.

Upo usemi kwamba kisichokuua kinakufanya kuwa imara zaidi, na hivyo ndivyo ilivyo kwa kila ugumu na changamoto unayokutana nayo kwenye maisha yako, kama inakuacha hai, basi jua inakuacha ukiwa imara zaidi ya ulivyokuwa kabla ya kukutana nayo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha