“A benefit should be kept like a buried treasure, only to be dug up in necessity. . . . Nature bids us to do well by all. . . . Wherever there is a human being, we have an opportunity for kindness.”
—SENECA, ON THE HAPPY LIFE, 24.2–3

Hongera sana mwanamafanikio kwa nafasi hii nyingine nzuri sana tuliyoiona leo.
Ni fursa nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari NAFASI YA KUFANYA WEMA…
Kila palipo na binadamu, pana nafasi ya kufanya wema.
Popote ulipo na kwa chochote unachofanya, kila unapokutana na binadamu mwingine, hiyo ni fursa nzuri kwako kutenda wema.
Na kadiri unavyowatendea wema wengine, ndivyo unavyoweza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

Na wajibu wako wewe ni kutenda wema, kuwahudumia vizuri wengine, kuwasaidia pale walipokwama na kuhakikisha kila anayekutana na wewe anaondoka akiwa bora kuliko alivyokuja.
Siyo wajibu wako kupima kama mtu huyo atakulipa wema huo au la,
Siyo kazi yako kudai watu wakulipe wema ambao umewafanyia.
Kilicho ndani ya uwezo wako ni kuwa mwema kwa kila mtu, watu hao kujibu wema huo haipo ndani yako na hivyo usiruhusu hilo likusumbue.

Kama ambavyo ng’ombe anatoa maziwa bila ya kutudai tulipe wema huo, kama ambavyo mwembe unatoa maembe bila kuangalia kama tumeshukuru au la na kama ambavyo nyuki wanaendelea kutoa asali hata kama hatujawashukuru, ndivyo na wewe unapaswa kuwa mwema kwa wengine, bila ya kuangalia kama wanashukuru au wanakulipa wema huo.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa mwema kwa kila unayekutana naye leo, kuhakikisha anabaki akiwa bora kuliko alivyokuwa. Kila fursa unayopata ya kumhudumia mteja wako leo, itumie kutenda wema.
#WemaHauozi #UsitakeKukipwaKwaWema #KilaAlipoMtuKunaFursaYaKutendaWema

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1