Anza kujiheshimu wewe mwenyewe.

Huwa tunataka wengine watuheshimu, watutambue kwa umuhimu wetu na mchango mkubwa tunaofanya.

Lakini je, sisi wenyewe tunajiheshimu? Sisi wenyewe tunajitambua kwa nafasi, umuhimu na mchango tulionao?

Kwa sababu chochote ambacho tunataka wengine watupe, huwa wanaanza kuangalia kama tunajipa sisi wenyewe kitu hicho. Kama tunajipa basi na wao wanatupa, lakini kama hatujipi na wao hawatupi.

Kama wewe ni kiongozi, bosi au mmiliki wa biashara, unaweza kuwaambia sana watu umuhimu wa kuwahi kazini, lakini kama wewe unachelewa, utatumia nguvu nyingi sana kwenye hilo. Lakini ukianza wewe kuwahi kazini, unafika kabla ya wote, huhitaji kutoa neno lolote, watu wataanza kuwahi.

Kama unatumia muda wako hovyo, kuutawanya kwa mambo yasiyo muhimu na kwa yeyote anayeutaka, watu wanajifunza kwamba muda wako hauna thamani. Hivyo watatumia kila fursa wanayoipata kutumia muda wako vibaya. Lakini kama unathamini muda wako, unausimamia kwa umakini na kuuweka kwenye yale mambo muhimu pekee, watu wanajifunza kutaka muda wako pale wanapokuwa na jambo muhimu kweli.

Na hata kwenye kuaminika na wengine, anza kujiamini kwanza wewe mwenyewe. Anza kutekeleza kila unachojipangia na kila unachoahidi mwenyewe na watu watakuamini kwa sababu hilo linaonekana na siyo kwa sababu umewaambia wakuamini.

Usikazane kuwaambia watu wakuchukulieje wewe, bali anza kujichukulia vile unavyotaka watu wakuchukulie na haitachukua muda watakuwa wanakuchukulia hivyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha