Siku moja ya April mwaka 2016 palikuwa na kusanyiko kubwa kwenye uwanja wa mpira wa shule ya Sacred Heart iliyopo Atherton, California nchini marekani. Katika kusanyiko hilo, walihudhuria watu wengi sana, lakini wengi zaidi walikuwa waanzilishi na wakurugenzi wa makampuni makubwa ya teknolojia duniani. Baadhi yao walikuwa; Larry Page na Sergey Brin (waanzilishi wa Google), Mark Zuckerberg (mwanzilishi wa Facebook), Sheryl Sandberg (mkurugenzi wa Facebook), Tim Cook (Mkurugenzi mkuu wa Apple), Jeff Bezos (Mwanzilishi wa Amazon). Wengine ambao pia ni wakurugenzi au viongozo wa makampuni makubwa ya teknolojia waliokuwepo kwenye kusanyiko hilo ni  Mary Meeker. John Doerr. Ruth Porat. Scott Cook. Brad Smith. Ben Horowitz. Marc Andreessen. Jonathan Rosenberg na Eric Schmidt.

Haijawahi kutokea viongozi wote hao wakubwa wakawa kwenye kusanyiko moja. Lakini kwa siku hiyo, wote walikusanyika kumuaga mtu ambaye alikuwa muhimu sana kwa ukuaji wa makampuni yao ya teknolojia waliyoanzisha. Mtu huyo aliitwa William Vincent Campbell, Jr. William au kama alivyoitwa kwa kifupi Bill, alikuwa kocha wa waanzilishi na wakurugenzi wa makampuni makubwa. Alifanya kazi kwa karibu na makampuni hayo tangu yanaanza, yanapitia changamoto na kukua. Makampuni kama Apple (inayotengeneza iphone), Google, Facebook, Intuit na mengine.

TrillionDollarCoach.jpg

Japokuwa Bill hakuwa maarufu na mtu aliyejulikana sana, aliheshimika sana na wale ambao waliwakochi katika kuendesha biashara zao. Alikuwa na misingi ambayo iliwasaidia sana katika kuendesha na kukuza biashara zao. Waanzilishi na wakurugenzi wa makampuni hayo makubwa, wanakiri kwamba kama isingekuwa Bill, makampuni yao yasingefika pale yalipofika sasa. Ukikusanya kwa pamoja makampuni yote ambayo Bill ameyakochi, thamani yake inazidi dola trilioni moja za kimarekani.

Pamoja na mafanikio haya makubwa katika ukocha, Bill hakupenda umaarufu. Alikwepa sana kuandikwa kwenye vyombo vya habari, na hata alipoombwa aandike kitabu hakukubaliana na wazo hilo. Walijitokeza waandishi ambao waliomba awape ushirikiano ili waandike kitabu kuhusu mafanikio yake, lakini hilo pia alilikataa.

Ni mpaka alipofariki, na siku ya kuagwa ambapo walihudhuria watu wengi mashuhuri, ndipo wakurugenzi wawili wa Google na ambao wamewahi kufanya naye kazi, Jonathan Rosenberg na Eric Schmidt walipofikiri na kuona kuna umuhimu wa watu wengine kushirikishwa misingi ya Bill ambayo iliwawezesha wao kufanikiwa sana. Na hapo ndipo walipokuja na wazo la kuandika kitabu, na kitabu hicho kupewa jina la Trillion Dollar Coach: The Leadership Playbook of Silicon Valley’s Bill Campbell. Kitabu hiki kimeshirikisha misingi ya ukocha ya Bill Campbell ambayo imeziwezesha kampuni za teknolojia kufanikiwa sana.

Kwenye makala ya TANO ZA JUMA tutakwenda kujifunza kwa kina misingi hiyo na kumjua zaidi Bill. Kwenye makala hii tutakwenda kujifunza tabia tano za watu wanaofundishika na ambao wana nafasi ya kufanikiwa sana.

Moja ya misingi ya Bill ilikuwa ni WAFUNDISHE WANAOFUNDISHIKA. Bill hakuwa anakubali kumkochi kila mtu, badala yake alimchunguza kwanza mtu na akigundua kwamba anafundishika basi alikubali kuwa kocha wake. Kama aligundua mtu huyo hafundishiki, hata kama angekuwa tayari kulipa gharama kiasi gani, hakukubali kuwa kocha wake.

SOMA; Sababu Tatu Kwa Nini Mafanikio Madogo Yanakuwa Sumu Ya Wewe Kufikia Mafanikio Makubwa Zaidi Na Jinsi Ya Kuziepuka.

Hapa tutakwenda kujifunza tabia hizo tano, ili wewe mwenyewe uweze kujipima na kuona uko wapi na pia uweze kuchukua hatua sahihi.

Kabla ya kuingia kwenye tabia hizi tano, nishirikishe kidogo uzoefu wangu kwenye eneo hili la ukocha. Nimekuwa nawakochi watu kwenye maeneo ya mafanikio kwa miaka mitano sasa, na katika kipindi hiki, nimeona baadhi ya watu wakifanikiwa sana na wengi wakishindwa, wapo ambao wanafanikiwa kidogo mwanzoni na hapo wanaridhika kitu kinachopelekea kushindwa baadaye. Baada ya kukutana na tabia hizi tano, nimeona jinsi ambavyo zina nguvu sana kwenye mafanikio ya watu. Hivyo zijue tabia hizi, na fanya uwezavyo kujijengea tabia hizi ili na wewe ufundishike na uweze kufanikiwa.

TABIA TANO ZA WATU WANAOFUNDISHIKA NA WENYE NAFASI YA KUFANIKIWA.

Zifuatazo ni tabia tano ambazo Bill Campbell aliziangalia kwa mtu kabla ya kukubali kuwa kocha wake. Jijengee tabia hizi ili uweze kufundishika na kufanikiwa zaidi.

MOJA; UAMINIFU.

Jukumu kubwa la kocha ni kumsaidia mtu kujijua yeye mwenyewe ili kuweza kuchukua hatua sahihi kwa mafanikio yake. Lazima mtu ajue uimara wake uko wapi na madhaifu yake yako wapi. Hili linahitaji uaminifu wa hali ya juu sana.

Hakuna mtu anayependa kukiri ana udhaifu kwenye eneo fulani. Na hilo ndilo limekuwa linachangia watu wengi kushindwa, kwa sababu hawakubali pale ambapo hawapo vizuri, hasa wanapokuwa waanzilishi au wakurugenzi wa makampuni makubwa.

Unapaswa kuwa mwaminifu kwako binafsi na kwa wengine kama kweli unataka kuwa mtu unayefundishika na utakayefanikiwa. Kujidanganya wewe wenyewe na hata kuwadanganya wengine kunaweza kukupa matokeo ya muda mfupi, lakini baadaye inakupelekea kwenye anguko kubwa.

Jijue vizuri wewe mwenyewe na pale wengine wanapokuonesha madhaifu uliyonayo, usiwakatalie na kuwaambia hawajui, bali angalia ni kwa namna gani ufanisi wako umekuwa kwenye maeneo hayo.

Hakuna mtu ambaye ana uimara maeneo yote, hakuna anayeweza kufanya kila kitu, hakuna anayejua kila kitu. Unavyoelewa na kukubali hilo haraka inakusaidia kuweka nguvu zako eneo sahihi na kuweza kufanikiwa.

MBILI; UNYENYEKEVU.

Unyenyekevu ni muhimu sana kwenye mafanikio. Tofauti na ilivyokuwa inachukuliwa zamani, kwamba kiongozi ni mtawala na yuko juu ya wengine wote, uongozi ni utumishi kwa wengine. Kiongozi anapaswa kuwahudumia wengine, na siyo kujiona yuko juu yao.

Bill aliangalia sana tabia hii ya unyenyekevu kwa wale waliotaka awe kocha wao, kwa sababu alijua kama tabia hii haipo, atakuwa anasaidia kutengeneza matatizo makubwa. Kiongozi asiyekuwa na unyenyekevu ni kiongozi ambaye kadiri anavyopata nguvu ndivyo anavyowaumiza wengi zaidi.

Jijengee tabia ya unyenyekevu, na hii haimaanishi uwe mpole na kuwa tayari kuonewa na wengine, bali uwe mtu wa kujishusha na kuwahudumia wengine, uwe tayari kushirikiana na wengine kwa ajili ya kupiga hatua zaidi.

Na kadiri unavyofanikiwa, ndivyo unyenyekevu unahitajika zaidi, kwa sababu wengi wanapofanikiwa hujiona wao ndiyo wanajua kila kitu na hakuna anayeweza kuwashauri au kuwakosoa. Viburi vya aina hiyo vimewagharimu watu wengi, wakaishia kuanguka vibaya baada ya kufanikiwa.

Unapokuwa mnyenyekevu unakuwa huna kiburi, unaweza kushirikiana na kila mtu na fursa za mafanikio zinakuwa nyingi zaidi kwako.

TATU; KUFANYA KAZI.

Haijalishi unafundishwa au kushauriwa na nani, kocha ni mtu wa kukupa mwongozo sahihi na kukuonesha pale unapokosea, ambapo siyo rahisi wewe mwenyewe kuona. Lakini sehemu kubwa ya mafanikio yako inategemea kiwango cha kazi unachoweka.

Lazima uwe tayari kufanya kazi sana ili kufanikiwa. Bill aliangalia watu ambao wapo tayari kujituma zaidi ya wengine, watu waliopenda kufanya kazi na siyo watu wa kutafuta njia za mkato za mafanikio. Hawa ndiyo aliokubali kuwakochi na waliweza kufanikiwa sana.

Je wewe unapenda kazi? Je unaamini kwenye kazi? Je upo tayari kuweka juhudi kubwa kuliko wengine wote? Upo tayari kufanya kazi wakati wengine wanapumzika na kustarehe? Kama majibu ni ndiyo basi upo kwenye nafasi nzuri ya kufanikiwa. Kama majibu ni hapana, na kama unajiambia huhitaji kufanya kazi kwa nguvu bali kwa akili, jua nafasi yako ya kufanikiwa ni ndogo sana.

Hatari kubwa zaidi ya mafanikio ipo kwa wale ambao wanaanzia chini, wanajituma sana na wanapata mafanikio kidogo. Wakishapata mafanikio hayo, wanaona hawahitaji kujitesa tena kama awali. Hawa ndiyo huwa wanaanguka vibaya sana. Haijalishi umefanikiwa kiasi gani, lazima uendelee kufanya kazi kwa nguvu na maarifa, lazima uendelee kujituma zaidi, hakuna wakati utajiambia umeshafika kileleni, kila wakati ni wa kujituma zaidi.

SOMA; Siri Pekee Ya Mafanikio Ambayo Hakuna Anayekusisitizia Kama Siri Nyingine.Siri Pekee Ya Mafanikio Ambayo Hakuna Anayekusisitizia Kama Siri Nyingine.

NNE; UVUMULIVU.

Hakuna mtu yeyote ambaye amewahi kupata kila anachokitaka kwa wakati anaoutaka. Hata ujitume kiasi gani, unaweza kufanya kila unachopaswa kufanya, lakini matokeo yakaja tofauti na ulivyotegemea. Hapa ndipo wengi hukata tamaa na kujiona hawana bahati ya kufanikiwa.

Kocha Bill alilijua hili na aliangalia sana tabia ya uvumilivu kwa wale ambao walitaka awakochi. Aliangalia watu ambao ni wavumilivu, ambao wapo tayari kuendelea hata pale wanapokutana na ugumu. Ambao wana ndoto na wapo tayari kuipigania bila ya kujali wanakutana na ugumu kiasi gani.

Jijengee tabia hii ya uvumilivu na ung’ang’anizi na kwa hakika utaweza kupata chochote kile unachokitaka kwenye maisha yako. Kadiri unavyovumilia na kung’ang’ana ndivyo dunia inavyokuheshimu na kuwa tayari kukupa chochote kile unachokitaka.

Kama ni mtu wa kujaribu kitu kwa muda mfupi na ukiona hakilipi unaenda kwenye kitu kingine, jua huna nafasi ya kufanikiwa. Jua kile unachokitaka kweli na ng’ang’ana nacho mpaka ukipate.

TANO; UTAYARI WA KUJIFUNZA.

Hakuna watu wagumu kufundisha na kushauri kama  wale ambao wanaamini tayari wanajua kila kitu. Hawa ni watu ambao hawajui, halafu hawajui kwamba hawajui. Hujiamini sana huku wakiwa hawana msingi sahihi, na hivyo huishia kushindwa.

Kocha Bill alilijua hili, alijua kuna watu wanaweza kuja kwako kuomba ushauri, lakini tayari wameshafanya maamuzi yao. Hivyo kama utawashauri kama wanavyotaka wanakubali na kufanyia kazi, ila kama utawashauri kinyume na wanavyotaka wao wanaona wewe hujui au hufai. Hivyo alichagua sana watu wa kuwakochi, kwa kuangalia utayari wa watu hao kwenye kujifunza. Mtu ambaye yupo tayari kujifunza na kuchukua hatua kwenye yale anayojifunza ana nafasi kubwa ya kufanikiwa. Lakini mtu ambaye anaona hana kipya cha kujifunza, huyo ameshaanza safari ya kuanguka.

Jijengee tabia ya kupenda kujifunza, kua tayari kujifunza kupitia kusoma vitabu, kuhudhuria semina na mafunzo mbalimbali, kupitia ushauri wa wengine na kwa uzoefu wako na wa wengine pia. Usipuuze au kudharau nafasi yoyote ya kujifunza. Na hata kama umefanikiwa, endelea na utayari wako wa kujifunza, huo ndiyo utakaokuwezesha ubaki kwenye mafanikio na hata kupiga hatua zaidi.

Rafiki, hizo ndizo tabia tano za watu wanaofundishika, ambao wana nafasi kubwa ya kufanikiwa kwenye maisha yao.

Swali langu kwako ni hili; je wewe unafundishika? Je wewe una tabia hizi tano? Jipe majibu ya ukweli kwa kuzingatia tabia ya kwanza ya uaminifu, na hayo yatakusaidia kuchukua hatua sahihi.

Siku moja nikiwa na baadhi ya wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, moja ya programu za ukocha ninazoendesha, walitaka kujua natumia vigezo gani mpaka kukubali kumkochi mtu. Niliwaeleza kigezo kikubwa ni utayari wa mtu kujifunza na kuchukua hatua. Kama mtu yupo tayari kujifunza, ukimshauri au kumwelekeza kitu anasikiliza na anaenda kuchukua hatua mara moja, basi huwa nakubali kumkochi mtu huyo, kwa sababu najua atakwenda kufanya makubwa. Lakini wale ambao ni watu wa sababu, watu wa kusubiri na kuona hawajawa tayari, huwa siwapi nafasi ya kuwakochi. Niliwashirikisha pia ya kwamba kwenye KISIMA CHA MAARIFA, kuna wanachama wapatao mia mbili, lakini lengo langu ni kuwa na wanachama 100 pekee, ambao wamejitoa kweli kufanikiwa. Najua nikiweka nguvu zangu kwa watu 100 waliojitoa kweli, wanaofundishika, tutaweza kuleta mabadiliko makubwa sana kwenye jamii zetu na nchi kwa ujumla.

Hivyo kama upo kwenye KISIMA CHA MAARIFA, jipime kwa tabia hizi tano, kama kuna ambayo huna, jijengee mara moja kwa sababu itakugharimu na itakufanya ukose nafasi ya kuendelea kuwa mwanachama.

Kama bado hujawa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, na umejipima na kuona una tabia hizo tano, unajichelewesha kufanikiwa. Unahitaji kuwa na kocha ili kufanikiwa, na mimi nakupa huduma hiyo kwa urahisi sana kupitia KISIMA CHA MAARIFA. Pata nafasi ya kuwa mwanachama leo kwa kutuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap namba 0717396253. Karibu sana.

SOMA; Karibu Kwenye Semina Ya Kisima Cha Maarifa 2019; Afya, Utajiri Na Hekima.

Usikose makala ya TANO ZA JUMA na #MAKINIKIA ambapo tutakwenda kujifunza kwa kina zaidi kuhusu umuhimu wa kuwa na kocha na misingi ya ukocha ya Bill Campbell ambayo iliwawezesha watu kufanikiwa zaidi. Ili kupata makala hizi, hakikisha umejiunga na channel ya TANO ZA JUMA ambayo ipo kwenye mtandao wa telegram. Maelezo ya kujiunga yako hapo chini. Yasome na uchukue hatua sasa.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu