Rafiki yangu mpendwa,
Nichukue nafasi hii ya kipekee sana kukupongeza kwa kuuanza mwaka huu mpya wa mafanikio 2019/2020. Hii ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuanza kuweka juhudi kubwa wakati wengine wameshapunguza kasi na wanasubiri mwaka 2020 uanze.
Kwa nini mwaka mpya wa mafanikio?
Kama unajiuliza huu mwaka mpya wa mafanikio ni nini na kwa nini unaanza mwezo novemba, basi nichukue nafasi hii kukupa ufafanuzi kidogo.
Watu wote huwa wanauanza mwaka mpya tarehe moja ya mwezi januari ya kila mwaka. Lakini huu ndiyo wakati ambao watu wanakuwa na hisia za juu za kuuona mwaka mwingine mpya, na kila mtu anakuwa anajiwekea malengo. Hivyo wengi hujikuta wakibeba malengo ambayo siyo yao, bali yale malengo ambayo wengine nao wanaweka. Mwezi mmoja baadaye wanakuwa wameshayasahau malengo yao.
Kwenye KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni familia ya wanamafanikio, watu ambao wamejitoa kujituma ili kufanikiwa zaidi, tunauanza mwaka mpya mapema kabisa kabla watu wengine hawajafanya hivyo. Tunajiwekea malengo na mipango na kuanza kuifanyia kazi wakati wengine wakiwa wameshapunguza kasi kwenye kipindi hiki cha mwisho wa mwaka na kusubiri mwaka mpya uanze ndiyo waanze tena.
Kwa kuuanza mwaka mpya miezi miwili kabla ya wengine, tunakuwa kwenye nafasi ya kupiga hatua kubwa zaidi ya wengine.
Mwaka wetu wa mafanikio 2019/2020 unakwenda kuanza leo tarehe 01/11/2019 mpaka tarehe 31/10/2020.
Tunakwenda kuuanza mwaka huu rasmi kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2019 ambayo itafanyika jumapili ya tarehe 03/11/2019 na hapo tutapata nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali na kila mmoja kujiwekea lengo moja ambalo atafanyia kazi kwa mwaka mzima na kushirikisha matokeo yake kila mwezi.
Huu ni mwaka wa kazi.
Rafiki yangu mpenda mafanikio, mwaka mpya wa mafanikio 2019/2020 ni mwaka wa kazi. Huu ni mwaka ambao kila mmoja wetu anapaswa kujituma zaidi kwenye kazi yake, biashara yake na chochote anachofanya, ili kutoa matokeo bora, ili kutoa thamani zaidi na hatimaye kuweza kulipwa zaidi.
Huu ni mwaka wa kujali sana muda wako, mwaka wa kutokuruhusu mambo yasiyo na tija kuchukua muda wako hata kama ni dakika chache.
Mwaka huu wa mafanikio 2019/2020, pima kila unachofanya kwa mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio ambao ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA. Kama kitu hakiboreshi afya yako, hakikuingizii fedha na hakikufanyi uwe na hekima zaidi, usikifanye. Ni hivyo tu na utaweza kupeleka muda na nguvu zako kwenye vile ambavyo ni sahihi kwako, na hivyo kuweza kupiga hatua sana mwaka huu.
Kwa mwongozo huo, vitu kama mitandao ya kijamii, kuangalia tv, kufuatilia habari za udaku na maisha ya wengine, kubishana siasa, dini na hata michezo na mengine kama hayo hayana nafasi kwetu kwenye mwaka wetu wa mafanikio 2019/2020.
Huu ni mwaka wa kazi, jitoe kuweka kazi zaidi na kwa hakika, hutabaki pale ulipo sasa. Kama ambavyo nimekuwa nakuambia, KAZI NDIYE RAFIKI WA KWELI, Kazi haimtupi yeyote anayeiheshimu na kuijali. Twende tukaweke kazi, tujijengee nidhamu ya kazi na tujitume zaidi kwa chochote tunachofanya.
Chochote tunachoruhusu mikono yetu ishikie, tuhakikishe tunaacha alama yetu kwenye kitu hicho.
Kauli mbiu; #Kipato Zaidi2020.
Ni nani asiyependa kipato zaidi? Mtu tajiri kuliko wote duniani, kila siku anaamka na kwenda kuweka kazi ili kukuza zaidi kipato chake. Hivyo sisi wanamafanikio wote, bila ya kujali hali yetu ya kipato kwa sasa, kila mmoja wetu anahitaji kipato zaidi.
Hivyo kauli mbiu yetu ya mwaka wa mafanikio 2019/2020 ni #KipatoZaidi2020. Chukua muda na kukokotoa kipato ambacho umeingiza kwa mwaka mmoja uliopita, kisha weka lengo la kuongeza zaidi kipato hicho kwa mwaka, kisha gawa kwa mwezi, kwa wiki na hata kwa siku. Kisha chukua hatua sahihi za kuongeza kipato hicho.
Kwa wale ambao watashiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2019, tutakwenda pamoja kwenye hatua hii ya kujiwekea lengo la kipato zaidi, kupata namba ambayo mtu utaifanyia kazi ili kuweza kufikia lengo la kipato zaidi analokuwa amejiwekea.
Kila mtu ana nafasi na fursa ya kuweza kukuza zaidi kipato chake zaidi ya pale kilipo sasa, unachohitaji ni kuwa na maarifa sahihi na kuchukua hatua sahihi ili kuweza kufikia hilo.
Code; #487/365NoDayOff
Rafiki yangu katika mafanikio, nimewahi kukushirikisha umuhimu wa kuwa na code (alama) ambayo unaitumia katika kuendesha siku zako na maisha yako kwa ujumla. Kwa muda mrefu nimekuwa natumia code #486 yaani kuianza siku ya kazi saa kumi asubuhi (4am) kuimaliza saa mbili usiku (8pm) kwa siku 6 za wiki na kuiacha siku moja isiyokuwa na ratiba kali. Lakini pia kila mwaka nimekuwa najipa likizo ya wiki moja ambapo najichimbia na kuzama kwa kina kwenye usomaji, tahajudi na kufikiri na kisha kuja na mpango wa kufanyia kazi mwaka mzima.
Mwaka huu wa mafanikio 2019/2020 nitabadili code na sasa itakuwa #487/365NoDayOff, ikimaanisha kuianza siku ya kazi saa kumi asubuhi, kuimaliza saa nne usiku kwa siku 365 za mwaka bila ya kuwa na siku ya mapumziko hata moja. Najua hili siyo rahisi, lakini kwa malengo makubwa niliyonayo, kama nitaendelea kwenda ninavyoenda sasa, kuyafikia itakuwa ni ndoto. Hivyo nahitaji kubadili baadhi ya vitu ili kwenda sawa na malengo makubwa ninayofanyia kazi.
Nakusihi na wewe rafiki yangu utengeneze Code yako itakayokuongoza kwa mwaka mzima, siyo lazima iwe kama yangu, chagua kitu ambacho unaweza kukifanyia kazi, lakini pia ikusukume zaidi, isikufanye uendelee kuwa kawaida.
Huduma ya KISIMA CHA MAARIFA kuwa kwa wachache.
Huduma ya KISIMA CHA MAARIFA ndiyo huduma kuu na ya kwanza kwa wale wote ambao wanataka kuwa karibu na mimi zaidi. Huduma hii imekuwa na msaada kwa wengi kuweza kupata mafunzo na hamasa ya kupiga hatua zaidi.
Kwa mwaka huu wa mafanikio 2019/2020, huduma hii itakwenda kubadilika kidogo, kwanza itakuwa kwa wachache sana. Kwa sasa huduma ina watu karibu 200, lakini wengi hawaiishi ile misingi ya KISIMA CHA MAARIFA, wengi wanaichukulia kawaida tu.
Lengo la mwaka wa mafanikio 2019/2020 ni kupunguza nafasi za watu kuweza kupata huduma hii, kutoka 200 mpaka kufika 100. Hivyo nitachagua kwa umakini sana nani anayeweza kuendelea na huduma hii, kulingana na matokeo anayopata kwenye maisha yake. Na kwa wale wapya watakaopenda kujiunga, kutakuwa na njia ya kuchuja kwanza jinsi gani mafunzo ninayotoa bure yamemsaidia kupiga hatua.
Hivyo kama tayari upo kwenye KISIMA CHA MAARIFA na ungependa kuendelea kuwepo, jikumbushe misingi ya KISIMA CHA MAARIFA na ifanyie kazi kila siku. Kama ni mgeni na unataka kujiunga na KISIMA, anza kufanyia kazi yale mafunzo ninayotoa nje ya KISIMA, soma vitabu ambavyo nimeandika, fanyia kazi na pata matokeo mazuri kisha omba nafasi ya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA na kupitia matokeo yako, utaipata.
Kwenye mwaka huu wa kazi 2019/2020, mfumo wa masomo kwenye KISIMA CHA MAARIFA utabadilika. Badala ya kuwa na semina mbili kubwa zinazoendeshwa kwa njia ya mtandao, kila wiki kutakuwa na mfululizo wa masomo yanayolenga kauli mbiu ya mwaka wetu wa mafanikio #KipatoZaidi2020 na #NidhamuYaKazi.
Karibu sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA, karibu sana tuwe karibu, tujitume zaidi na kuweza kupiga hatua zaidi.
Klabu za KISIMA CHA MAARIFA.
Kwenye mwaka wa mafanikio 2018/2019 tumefanikiwa kuanzisha klabu za KISIMA CHA MAARIFA karibu mikoa yote ya TANZANIA. Tumeweza kuwa na klabu zinazofika 20. Klabu zitakuwa kiungo maalumu na kipaumbele cha kwanza katika kupata nafasi ya kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA.
Hivyo mwaka wa mafanikio 2019/2020 tunakwenda kuweka juhudi kubwa kwenye klabu zetu, kwa sababu kwa muda mchache ambao tumezifanyia kazi, zimeonesha kuwa na manufaa makubwa.
Pia klabu za KISIMA CHA MAARIFA zitakuwa ndiyo sehemu ya watu kupata nafasi ya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Mtu atakayeomba kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, ataelekezwa kwanza kushiriki kwenye klabu iliyo karibu yake, kuipata misingi na kuona mambo yanavyokwenda na kisha kupata nafasi ya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.
Tuendelee kuweka juhudi kubwa kwenye klabu zetu ili tuweze kupiga hatua zaidi.
Nafasi za huduma za ukocha.
Mwaka wa mafanikio 2018/2019 tumejaribu huduma mbili kuu za ukocha GAME CHANGERS na LEVEL UP na zimekuwa na matokeo mazuri kwa wale walioshiriki na kuchukua hatua.
Mwaka wa mafanikio 2019/2020 tunakwenda kuweka nguvu kubwa zaidi kwenye programu hizo mbili za ukocha.
Kutakuwa na misimu mitano ya huduma ya GAME CHANGERS, hivyo nafasi za kushiriki zitakuwa 25 kwa mwaka mzima. Maelezo zaidi ya hili yatatolewa.
Kwa upande wa programu ya LEVEL UP, ambayo inawalenga wale ambao tayari wana biashara na wanataka kupiga hatua zaidi (LEVEL UP) kutakuwa na nafasi 12 za kushiriki. Hii ni programu inayoendeshwa kwa majuma 50 ya mwaka na kila juma unaripoti maendeleo ya biashara yako pamoja na kupata masomo muhimu ya kukuwezesha kukuza biashara yako zaidi.
Huduma kuu #2020Vitabu150Watu1000
Rafiki, huduma kuu ambayo nitakwenda kuiwekea nguvu zaidi ni kwenye kuhamasisha na kushirikisha usomaji wa vitabu. Hiki ni kitu ambacho nimeona kinaweza kuwa na matokeo makubwa kwa wengi na kwa gharama ndogo.
Ninafanya tathmini ya vitabu ambavyo nimeshasoma mpaka sasa, na bado naendelea kuviorodhesha, nimeshaorodhesha zaidi ya vitabu 400 na bado sijavimaliza. Kwa wastani nimekuwa nasoma vitabu 100 kwa mwaka. Sasa nakwenda kuongeza kiwango hicho mpaka kufika vitabu 150 kwa mwaka.
Hapo unaona kwa nini nakuambia mwaka 2019/2020 utakuwa mwaka wa kazi, na kwa nini huduma nyingine zinabadilika. Utakapoanza mwaka wa kalenda 2020, nitaanza kufanyia kazi lengo hilo rasmi, kusoma vitabu 150 ndani ya majuma 50, hapo ni sawa na vitabu 3 kwa kila wiki.
Nitakwenda kubadili huduma ya TANO ZA JUMA kuwa huduma ya SOMA VITABU TANZANIA. Hivyo nitashirikisha vitabu na chambuzi hizo kupitia channel ya telegram na ada itakuwa ile ile ya TANO ZA JUMA ambayo ni tsh elfu 1 kwa wiki au elfu 3 kwa mwezi au elfu 30 kwa mwaka. Kwa wale ambao wanataka kupiga hatua kweli, basi huduma hii itawafaa sana.
Nimekuwa naona wengi wanashindwa kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA kwa sababu ya ukubwa wa ada na kutokuwepo kwa mpango wa kulipa kwa awamu. Na sina mpango wowote wa kupunguza ada ya KISIMA CHA MAARIFA, badala yake napanga kuiongeza zaidi, ili wale wanaochagua kuingia kwenye huduma hiyo, wawe wamejitoa kweli na kuwa tayari kuchukua hatua kubwa.
Lakini kwenye huduma hii ya usomaji na uchambuzi wa vitabu, inamfaa kila mtu, kwa sababu kama unasoma hapa, maana yake una kompyuta au simu janja na umenunua kifurushi kwenye mtandao wa simu. Hivyo hukosi elfu moja kwa wiki, na hivyo unaweza kulipia huduma hii bila shaka kama kweli umejitoa kujifunza.
Karibu twende pamoja kwenye safari hii ya kusoma na kuchambua vitabu 150 kwa mwaka.
Rafiki, hayo ndiyo mambo makubwa ambayo tunakwenda kuyafanyia kazi kwenye mwaka wa mafanikio 2019/2020 ambao tumeuanza leo. Kama unataka twende pamoja kwenye safari hii ya mafanikio, basi naomba kitu kimoja kwako, kata shauri kwamba umeikubali safari hii ya mafanikio na upo tayari kulipa gharama. Na ukishafanya hivyo, basi naomba uwe unafundishika, kama tulivyojifunza sifa za kufundishika kwenye makala hii; Je Unafundishika? Tabia Tano Za Watu Wanaofundishika Na Wenye Nafasi Ya Kupata Mafanikio Makubwa. Pamoja na mambo matatu niliyokuomba uwe nayo ili twende pamoja kwenye KISIMA CHA MAARIFA kwenye makala hii; 1756; Vitu Vitatu Ninavyohitaji Kutoka Kwako Ili Tuweze Kwenda Pamoja…
Naamini tutakwenda pamoja rafiki yangu, na ninaamini hakuna kinachoweza kutuzuia tusifikie mafanikio makubwa tuliyopanga kufikia.
Nakupenda sana rafiki yangu, na nimeyatoa maisha yangu kwa ajili yako, kwa sababu msingi mkuu wa mafanikio ninaouishi ni huu; UNAWEZA KUPATA CHOCHOTE UNACHOTAKA, KAMA UTAWASAIDIA WENGI ZAIDI KUPATA KILE WANACHOTAKA. Njoo tushirikiane pamoja ili ufanikiwe na mimi nitafanikiwa zaidi. Kama wewe hutafanikiwa, na mimi sitafanikiwa pia.
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha