Mimi siyo muumini wa kulalamika au kuwalaumu wengine. Mimi ni muumini wa kuchukua hatua, kama kuna kitu sikipendi basi nakibadili na kama siwezi kukibadili basi naachana nacho na kufanya mambo mengine.
Lakini kuna wengi wanapenda kulalamika, na wanajishawishi kwamba wana haki ya kulalamika, kwa sababu labda wameonewa, wamedhulumiwa au kufanyiwa chochote kile ambacho siyo haki.
Lakini pia wapo wale ambao wanachukua hatua ambazo wanajua kabisa zitaleta matokeo fulani, halafu wanapopata matokeo hayo wanalalamika. Hawa ndiyo huwa wananishangaza sana.
Yaani kuna hatua unachukua, na unajua kwa kuchukua hatua hiyo kuna matokeo utakayoyapata, halafu ukipata matokeo hayo unalalamika! Kweli?
Unajua kabisa ya kwamba mafanikio ni matokeo ya kuweka kazi sana, kutoa thamani kubwa kwa wengine. Na unajua kabisa ya kwamba wewe ukiwa kazini unatafuta kila njia ya kukwepa majukumu, unajua kabisa kama ungekuwa ndiyo mwajiri, usingeweza kumwajiri mtu wa aina hiyo. Lakini inapotokea wenzao wanapanda vyeo na kuongezewa mishahara huku wewe ukibaki pale ulipo unalalamika. Unakuwa unategemea nini?
Unajua kabisa ya kwamba wateja wanataka kitu kilicho bora na wanataka huduma nzuri. Wewe kwenye biashara yako umeweka vitu visivyo bora na huduma zako ni mbovu, unakazana kuwashawishi wateja waje kwenye biashara yako, wanakuja mara moja ila hawarudi tena, unakazana kulalamika kwamba wateja wako hawafai. Unafikiri wateja wana wajibu wa kununua kwako?
Unajua kabisa ya kwamba mahusiano yoyote yale yanajengwa na kuimarishwa kwa mawasiliano. Ila wewe kuna mambo unafanya na hujamshirikisha mwenzako, halafu mwenzako huyo anaanza kuwa na wasiwasi na wewe na mahusiano yanaingia kwenye mgogoro, unaanza kulalamika kwamba mwenzako hakuelewi. Atakuelewaje wakati hujachukua muda wa kumwelewesha?
Kila hatua unayochukua au kutokuchukua kwenye maisha yako, inachangia kwenye matokeo ambayo unayapata. Hivyo kabla hujalalamikia matokeo unayoyapata, anza kujiuliza ni hatua ipi uliyochukua imezalisha matokeo hayo. Fanyia kazi zile hatua unazochukua na utapata matokeo ya tofauti.
Kumbuka malalamiko ni sehemu ya kujifariji tu, lakini hayaleti matokeo ya tofauti kama hutachukua hatua za tofauti.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Tangu nimejiunga Kisima cha maarifa kwangu imenisaidia sana kupunguza na kuacha kulalamika na kuweka kazi mbele
LikeLike
Vizuri sana Beatus.
LikeLike
Asante Coach! Kulalamika ni mwanzo wa kushindwa, na ni kutafta kichaka cha kujificha ili kuleta sababu, kitu ambacho hakitakiwi. 🙏🙏
LikeLike
Kabisa,
Hatupaswi kujificha,
Tunapaswa kukabiliana na kila kinachotujia.
LikeLike