Tunapofikiria mafanikio kwenye maisha yetu, huwa tunafikiria mambo makubwa sana.

Na kila tunapoyaangalia mambo hayo, huku tukiangalia pale tulipo sasa, huwa tunaona ni vigumu kufika pale. Tunakosa kabisa hata nguvu ya kuanza, kwa sababu tunakuwa hatujui tunaanzia wapi.

Mara zote nimekuwa nakuambia ufikiri makubwa, lakini uanze kwa hatua ndogo. Hii ni kwa sababu hatua ndogo ndizo zinazoleta matokeo makubwa.

Ipo kauli maarufu kwamba hata mbuyu uliana kama mchicha, ni kauli tuliyoizoea, ila ina funzo kubwa sana, kwamba haijalishi unataka kufika mbali na juu kiasi gani, lazima uanze kidogo.

Pamoja na kujua umuhimu wa kuanza kidogo, bado wapo wengi huja na swali sasa naanzia wapi? Ndiyo, nipo tayari kuanza kidogo, lakini kidogo kipi nianze nacho?

Na leo nakwenda kukushirikisha hatua ndogo unazoweza kuanza kuzichukua sasa hivi hapo ulipo na zikakuletea matokeo makubwa sana baadaye.

Anza kwa kuwa mwema kwa mtu mmoja leo, iwe ni mteja wako, mfanyakazi mwenzako, mwenza wako au yeyote, anza kwa kuwa mwema kwa mtu mmoja tu, kwa kujali zaidi kuhusu yeye, kwa kuwa tayari kumsaidia pale alipokwama. Ukishafaulu kwa mmoja nenda kwa mwingine na mwingine na mwingine, muda siyo mrefu utakuta watu wengi wanakutegemea sana kwenye kile unachowasaidia.

Anza kwa kujifunza kitu kipya leo, kupitia usomaji na hata kujiangalia mwenyewe na wengine pia. Kwa kila unachojifunza, jiulize unawezaje kukitumia kwenye maisha yako na yakawa bora, kisha anza kukifanyia kazi. Fanya hivyo leo na kila siku, na kadiri unavyojifunza na kujaribu vitu vipya, utajiona ukikua zaidi. Jifunze mbinu za ushawishi na mauzo na anza kuzitumia kwa chochote unachofanya au kuuza.

Nenda hatua ya ziada kwenye kila unachofanya, kama kuna kazi unaifanya, nenda zaidi ya unavyotegemewa kufanya, kama una wateja unawahudumia, wape zaidi ya wanavyotegemea kupokea. Siyo lazima kiwe kitu kikubwa sana, ila kinapaswa kuwa kitu ambacho kitakutofautisha kabisa na wengine. Kwa kufanya hivyo kwa kila unayekutana naye, haitachukua muda watu watakuwa wanakuja zaidi kwako kwa sababu wanajua watapata zaidi.

Rafiki, hatua hizi ni ndogo sana, na ukizifanya mara moja huwezi kuona utofauti wake kwenye maisha yako, tena unaweza ukadharau kabisa. Lakini unaporudia rudia kufanya kwenye kila siku ya maisha yako, unajijengea sifa mpya, sifa ambayo itawavuta wengi zaidi kuja kwako, sifa ambayo itakuwezesha kufika mbali zaidi.

Huna cha kusubiri, anza sasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha