Kuna kitabu kimoja kifupi na kizuri sana ambacho kinaelezea tabia yetu sisi binadamu kuyapinga mafanikio.
Kitabu hicho kinaitwa WHO MOVED MY CHEESE, ambacho kinaeleza hadithi ya panya wanne ambao walizoea kupata jibini kwenye eneo walilozoea, siku moja wakaenda eneo hilo na kukuta hakuna tena jibini. Kuna ambao walisonga mbele na kutafuta jibini nyingine, lakini wapo ambao waliendelea kung’ang’ana pale pale wakiamini jibini haipaswi kupotea, bali inapaswa kubaki kama walivyozoea.
Hii ndiyo tabia ambayo sisi binadamu tunayo, tunapokutana na kitu kizuri, huwa tunataka kitu hicho kiendelee kuwepo kama tunavyotaka sisi wenyewe.
Iwe ni kwenye ajira, kujiajiri au biashara, huwa tunajisahau haraka sana tunapokutana na hali nzuri. Kwenye ajira mtu anapata kazi inayomlipa vizuri na kujisahau, kuamini kwamba kazi hiyo itaendelea kuwepo siku zote. Siku moja anapewa taarifa kwamba kazi hiyo haipo tena, anajikuta kwenye hali ya kushindwa kukubaliana na hilo kwa sababu hakuwa na maandalizi.
Hata kwenye biashara zetu, tumekuwa tunajisahau sana. Mtu unapata wazo la biashara, la utofauti na wengine wanavyofanya, hivyo unapata wateja wengi na faida nzuri, unajisahau na kuona umeshapatia biashara. Siku unakuja kustuka huna tena wateja kama zamani, unagundua watu wengine nao wamefungua biashara kama yako na kuchukua sehemu kubwa ya wateja wako.
Kama tumepata nafasi nzuri kwenye maisha yetu na hatutaki kuipoteza, basi hatua ya kwanza tunayopaswa kuichukua ni kutokujisahau kwenye nafasi hiyo. Kila wakati kuwa na maandalizi iwapo nafasi hiyo itapotea basi uwe na mbadala. Na muhimu zaidi, kila wakati unapaswa kuwa mbunifu na kuja na vitu vipya na bora zaidi vitakavyokufanya uendelee kuwa mbele ya wengine.
Mafanikio ni safari ambayo haina mwisho, ni vita ambayo haina kupumzika, kila siku ni nafasi ya wewe kujiboresha zaidi, nafasi ya wewe kujiandaa zaidi na kupiga hatua zaidi.
Siku utakayojiambia umeshafika juu na huna hatua zaidi za kupiga, hiyo ndiyo siku ambayo unakuwa umeanza kuporomoka. Usikubali kufika hatua hii kama unataka kuwa na maisha ya mafanikio wakati wote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,