“Aren’t you ashamed to reserve for yourself only the remnants of your life and to dedicate to wisdom only that time can’t be directed to business?”
—SENECA, ON THE BREVITY OF LIFE, 3.5b

Ni siku nyingine nzuri, siku mpya na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi hii nyingine bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari USIJIACHIE MAKOMBO…
Unashindwa kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako kwa sababu hujaweka vizuri vipaumbele vyako.
Upo tayari kutawanya muda wako kwa mambo ya nje, kama kazi, mitandao ya kijamii, tv, umbeya na mengine, lakini utajiambia husomi vitabu kwa sababu hupati muda.
Inakuwaje unaweza kupata muda wa kulala kila siku, kula mara tatu, kufuatilia maisha ya wengine, kufuatilia habari mbalimbali, lakini ukose muda wa kujiendeleza wewe binafsi kwa kujifunza na kujisokea vitabu?

Jibu ni kwa sababu umezoa kujiachia makombo.
Badala ya kutenga muda kwa jukumu hilo muhimu la maendeleo binafsi, wewe unajiambia utafanya ukipata muda.
Yaani ni sawa na kuandaa chakula kizuri, kisha kuwagawia wengine kwanza na kama kitabaki basi wewe ndiyo utakula.
Wote tunajua changamoto ya muda, kama usipoupangilia vizuri basi unapotea bila ya wewe kujua.

Hivyo leo nenda kaweke vipaumbele vyako vizuri, yape muda yale mambo ambao ni muhimu zaidi kwako na yanakusukuma kuwa bora zaidi.
Usitegemee makombo ya muda yatakayobaki ndiyo upeleke kwenye mambo hayo muhimu.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutenga muda kwa yale mambo muhimu na siyo kutegemea muda upatikane wenyewe. Usitegemee makombo ya muda kwenye vitu muhimu kama maendeleo yako binafsi.
#WekaVipaumbeleVizuri #MaendeleoBinafsiNdiyoKipaumbeleKikuu #KuwaBahiliWaMudaWako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1