“The human being is born with an inclination toward virtue.”
—MUSONIUS RUFUS, LECTURES, 2.7.1–2
Hongera sana mwanamafanikio kwa kupata nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni fursa bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari ULIZALIWA UKIWA MWEMA…
Sisi binadamu, kwa asili tunazaliwa tukiwa wema,
Wema ndiyo kitu pekee kilichoiwezesha jamii ya wanadamu kuendelea kuwepo hapa duniani mpaka sasa.
Na ukitaka kudhibitisha hili, waangalie watoto wadogo, mioyo yao ni safi, wapo tayari kushirikiana (kucheza) na watoto wengine muda mfupi baada ya kukutana.
Watoto wadogo hawakai na vinyongo, watakwazana na wenzao lakini dakika chache baadaye michezo inaendelea, bila ya kinyongo kwamba wewe ulifanya hivi.
Ni nadra sana kukuta watoto wadogo wakiwa na msongo wa mawazo au magonjwa mengine ya akili.
Lakini tunapofika utu uzima, kila aina ua ubaya tunaukaribisha,
Wivu, vinyongo, kuwatakia wengine mabaya, msongo wa mawazo na mengine mengi.
Unaweza kusema watoto hawapati vitu hivyo kwa sababu bado hawajajielewa na kuyaelewa maisha, lakini nakuambia wewe unapata vitu hivyo kwa sababu uujajielewa na kuyaelewa maisha, hasa kanuni za asili.
Kazi ya falsafa ni kutusaidia kurudi kwenye mstari, kutusaidia kurudi kwenye asili yetu, kutusaidia kuwa wema tena.
Pale tunapojikuta tumekasirika, tuna vinyongo, tuna msongo na mengine kama hayo, tunapaswa kujikumbusha hatua sahihi kwetu kuchukua ili kuondokana na hali hizo.
Umezaliwa ukiwa mwema, usikubali mazingira na wanaokuzunguka kukufundisha ubaya. Tumia falsafa kujitafakari kila wakati na kuchukua hatua sahihi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kurudi kwenye asili yako kama mwanadamu, asili ya kuwa mtu mwema na kushirikiana vizuri na watu wengine.
#WemaNiAsiliYako #UbayaUmefundishwa #FalsafaNiMwongozoWaKuturekebisha
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1