“Just as we commonly hear people say the doctor prescribed someone particular riding exercises, or ice baths, or walking without shoes, we should in the same way say that nature prescribed someone to be diseased, or disabled, or to suffer any kind of impairment. In the case of the doctor, prescribed means something ordered to help aid someone’s healing. But in the case of nature, it means that what happens to each of us is ordered to help aid our destiny.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 5.8.

Ni bahati iliyoje kwetu sisi kupata nafasi ya kuiona siku hii nyingine mpya ya leo.
Ni siku bora na ya kipeke sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUFUATA MAELEKEZO YA DAKTARI…
Unapoumwa, unakwenda kwa daktari, unamweleza yale yanayokusumbua, anakusikiliza, anakupima na kisha anakupa maelekezo ya namna matibabu yako yatakavyokwenda.
Haya ni maelekezo ambayo kila mtu huwa anayachukua kwa umakini mkubwa.
Kunywa dawa hii, vidonge viwili kutwa mara tatu na utafanya hivyo, japo dawa inaweza kuwa chungu, lakini unayafuata maelekezo ya daktari.
Usinywe pombe unapotumia dawa hii, na hata kama ni mlevi wa kupindukia utafuata maelekezo hayo.
Unafuata maelekezo ya daktari kwa sababu unajua anajua kuhusu ugonjwa wako kuliko wewe, na chochote anachokuambia ni kwa manufaa yako.

Lakini yupo daktari mkuu, ambaye naye huwa anatoa maelekezo yake, ambayo yana nia njema kwetu, lakini tumekuwa hatuyafuati maelekezo hayo.
Daktari huyu ni asili.
Asili huwa inatupa maelekezo kila mara, kupitia matokeo ambayo tunayapata,
Lakini badala ya kusikiliza maelekezo hayo na kuyafanyia kazi, huwa tunayakataa, huwa tunalalamika na kuona kama tunaonewa au tuna bahati mbaya.

Asili inaweza kukupa ugonjwa, kilema, kushindwa, kukataliwa,
Yote haya yanaumiza, lakini yana manufaa ndani yake. Kama ambavyo dawa ni chungu au sindano inauma lakini inatibu, ndivyo pia maelekezo ya asili yalivyo, yanakuumiza lakini yanakuja na manufaa makubwa ndani yake.
Jukumu lako ni kuyapokea maelekezo ya asili kama unavyopokea maelekezo ya daktari na kuyafanyia kazi. Na kwa hakika utakuwa na maisha bora sana.

Jua kila kinachotokea kwenye maisha yako, kimekuja kwa kusudi maalumu la kukufanya wewe kuwa bora zaidi, hata kama kinaumiza.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kupokea maelekezo ya asili na kuyafanyia kazi kama unavyopokea maelekezo ya daktari.
#AsiliHaikosei #KilaKinachotokeaKinaManufaaKwako #TafutaUzuriKwenyeKilaJambo

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1