Watu wengi wamekuwa wanapanga kuingia kwenye biashara, lakini ni wachache sana ambao huchukua hatua ya kuingia kwenye biashara kweli.

Wengi hujipa sababu kwa nini hawawezi kuingia kwenye biashara kwa wakati waliopanga, na sababu kubwa huwa ni kwamba hawajawa tayari.

Mtu anaweza kujiwekea lengo kabisa kwamba mwaka kesho ataingia kwenye biashara. Lakini wakati wa kufanya hilo unapofika, anakuja na sababu ambazo zinamzuia kuchukua hatua hiyo. Anaweza kujiambia hana mtaji, au hajafanya utafiti wa kutosha kwenye soko au hana muda wa kutosha kusimamia biashara yake.

Kinachotokea ni mtu kuahirisha mpango wake huo na kuusogeza mbele zaidi. Na hata baada ya kusogeza mpango wake mbele, bado anaendelea kuahirisha.

Wale unaowaona wapo kwenye biashara na wamefanikiwa, siyo kwamba walianza wakiwa wameshakamilisha kila kitu. Wengi walianza wakiwa hawajawa tayari na kipindi cha mwanzo walikutana na changamoto nyingi sana. Lakini kwa sababu walishafanya maamuzi ya kuingia kwenye biashara, walipambana mpaka wakafanikiwa.

Wengi ambao wameingia kwenye biashara na kufanikiwa, wanashukuru kwa kuanza kabla hawajawa tayari, wanakiri kama wangeendelea kusubiri mpaka wawe tayari kwenye kila kitu, wasingeingia kwenye biashara kamwe.

fred deluca subway.jpg

Fred DeLuca ambaye alikuwa mwanzilishi wa migahawa inayouza vyakula vya haraka (Subway) anatushirikisha jinsi alivyoingia kwenye biashara kabla hajawa tayari, akakutana na changamoto nyingi lakini kwa kupambana nazo akaweza kufanikiwa.

Fred anatuambia kilichomsukuma kuingia kwenye biashara ilikuwa ni kupata ada ya kujisomesha chuo. Kwa sababu wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumlipia ada, alikuwa akijishughulisha mwenyewe kwenye vibarua mbalimbali. Lakini kipato alichokuwa anaingiza kupitia vibarua, kisingetosha kuweza kumlipia ada ya chuo. Hivyo alienda kwa rafiki wa baba yake, aitwaye Pete, ambaye alikuwa na uwezo kidogo maana alikuwa mwajiriwa, akamuomba ushauri anawezaje kupata ada ya chuo.

Fred anasema wakati anaomba ushauri huo, kwenye mawazo yake alitegemea rafiki huyo angemkopesha fedha ili aje kulipa baadaye. Lakini alichomwambia ni kwa nini usianzishe biashara? Fred alimuuliza kwa mshangao, biashara gani? Ndipo Pete akamwambia kwamba amesoma kwenye gazeti kuna mtu anafanya biashara ya migahawa na ana migahawa 32 licha ya kuwa alianza kwa hatua ndogo sana.

Fred alifikiria hajawahi kufanya biashara yoyote na hata huyo Pete anayemshauri aingie kwenye biashara hajawahi kufanya biashara bali tu amesoma kuhusu mtu aliyefanikiwa kwenye biashara. Alianza kumweleza Pete kwamba hilo halitawezekana kwa sababu hana uzoefu wala mtaji. Pete akamjibu nipo tayari kuwa mshirika wako, na nitakupa mtaji wa kuanza.

Kwa nafasi hiyo ya kupata mtaji, Fred aliona hana cha kupoteza, hivyo alikubali kuingia kwenye biashara, huku akiwa hajui chochote kuhusu biashara hiyo. Baada ya kukubaliana kuingia kwenye biashara pamoja, Pete alimwambia Fred ni lazima wajiwekee lengo, na kupitia hamasa aliyoipata baada ya kusoma mtu mwingine aliyefanikiwa, waliweka lengo la kuwa na migahawa 32 ndani ya miaka kumi, lengo ambalo hawakujua hata watalifikiaje, lakini walijiwekea lengo hilo.

SOMA; Hatua Za Kuanza Na Kidogo Ulichonacho Hadi Kufikia Mafanikio Makubwa.

Walianza kutafuta eneo la kufanyia biashara yao, na kwa sababu mtaji walioanza nao ulikuwa kidogo, hawakuweza kumudu maeneo mazuri. Hivyo walipata eneo ambalo halikuwa sehemu nzuri ambayo watu wanapita. Baada ya kupata eneo, walianza kufanya utafiti kwa kwenda kula kwenye migahawa mingine inayotengeneza vyakula vya haraka. Walienda kama wateja lakini walitumia kila fursa kuchunguza jinsi ambavyo migahawa hiyo inaendeshwa, jinsi vyakula vinavyoandaliwa na mengine mengi.

Baada ya utafiti huo mfupi, mwaka 1965 walifungua mgahawa wao wa kwanza, kwa mtaji mdogo wa dola elfu moja pekee. Siku ya kwanza ya ufunguzi ilikuwa nzuri sana, watu walikuwa wengi kiasi cha kushindwa kuwahudumia. Walipata matumaini kwamba biashara hiyo ni nzuri na watafanikiwa sana. Lakini hawakuwa sahihi, kadiri siku zilivyokwenda ndivyo wateja walivyopungua na kipato kuwa kidogo. Biashara ilianza kujiendesha kwa hasara.

Kwa bahati nzuri sana, Pete n Fred walikuwa na utaratibu wa kuwa na kikao cha kibiashara kila siku ya jumatatu usiku. Siku hiyo walipita namba muhimu walizokuwa wanafuatilia kwenye biashara yao, hasa mauzo, idadi ya wateja na faida. Walipoona kila wiki wateja na mauzo vinapungua, waliona kuna umuhimu wa kuchukua hatua za haraka. Walijifunza vitu vingi sana ambavyo hawakuwa wanavijua awali. Walifanya makosa mengi kwa kutokujua, lakini kwa sababu walikuwa wameshaingia kwenye biashara, hawakuwa na budi bali kukabiliana na kila wanachokutana nacho.

Baada ya kuona mgahawa mmoja walionao hajiendeshi vizuri, walipata wazo la kufungua mgahawa mwingine. Hili lilikuwa wazo la ajabu ambalo kama wangesema wanaenda kuomba mkopo benki, hakuna benki ambayo ingeweza kuwakubalia. Yaani mgahawa wa kwanza unaendeshwa kwa hasara, halafu wanataka kufungua mgahawa mwingine? Kwa falsafa ya Fred ya anza kabla hujawa tayari, walianzisha mgahawa mwingine, na hapo mauzo yalianza kupanda. Wakaanzisha mwingine wa tatu na mauzo yakazidi kupanda zaidi.

Miaka nane baadaye tangu waingie kwenye biashara, walikuwa wamefanikiwa kufungua migahawa 16 pekee. Lengo lao ilikuwa ni kufungua migahawa 32 ndani ya miaka kumi. Kwa miaka 2 iliyobaki aliona hawezi kufungua migahawa mingine 16. Hivyo walifikiri kwa kina na kuja na wazo la kutoa kibali kwa watu wengine kuendesha mgahawa kwa mfumo wao (franchise). Japokuwa hawakuwa wanajua chochote kuhusu aina hiyo ya uendeshaji wa biashara, waliona ndiyo sahihi kwao kufikia lengo. Walikutana na changamoto nyingi mwanzo, lakini maamuzi hayo yaliwasaidia sana. Kwani miaka 11 tangu waingia kwenye biashara walikuwa wamefungua migahawa 32, miaka 2 baadaye migahawa 100 na miaka mitano baada ya migahawa hiyo 100 walikuwa wamefungua migahawa 200.

Fred anatushirikisha mengi sana kuhusu safari yake ya kuingia kwenye biashara kabla hajawa tayari, kuweka malengo makubwa na kujisukuma kuyafikia na kuweza kuukuza sana mgahawa wa Subway. Kwa sasa mgahawa huu umesambaa dunia nzima na hata hapa Tanzania migahawa hii ipo.

Fred anakiri kwamba kama angesubiri mpaka awe tayari, asingeweza kuingia kwenye biashara hii ya mgahawa. Anasema baada ya kuingia alikutana na vitu vingi ambavyo hakuvijua kuhusu biashara ya mgahawa, lakini kwa kuwa alishaingia hakuwa na namna bali kukabiliana navyo.

Na hivi ndivyo tunavyopaswa kuwa kama tunataka kuingia kwenye biashara na kufanikiwa. Kama bado hujaingia kwenye biashara, basi anza kabla hujawa tayari. Chagua sehemu yoyote unayoweza kuanzia, anza kidogo na anza na tatizo ambalo tayari watu wanalo na wapatie suluhisho la tatizo hilo. Utakutana na changamoto nyingi, lakini usikubali kukwama, kabiliana nazo na songa mbele.

Kama tayari upo kwenye biashara, jiwekee malengo makubwa zaidi ya yale unayofanyia kazi kwa sasa. Malengo ambayo watu wengine wataona ni makubwa na hayawezekani, kisha jisukume kuyafikia. Usisubiri mpaka uwe tayari, badala yake anza sasa, jiwekee lengo kubwa na anza kulifanyia kazi mpaka ulifikie.

Fred ametushirikisha masomo 15 aliyojifunza kwenye biashara kwenye kitabu chake kinachoitwa Start Small Finish Big; Fifteen Key Lessons to Start—and Run—Your Own Successful Business. Kwenye kitabu hiki ameshirikisha mifano ya wajasiriamali ambao walianza kwa mitaji midogo kabisa, wakaweka juhudi kubwa na baadaye wakaishia kuwa na biashara ambazo ni kubwa.

Masomo 15 yaliyopo kwenye kitabu hiki yanagusa kila eneo la biashara, kuanzia wazo la biashara, maono ya biashara, mtaji, kukabiliana na changamoto na wakatisha tamaa, kuongeza faida na mengine mengi.

Kwenye makala ya TANO ZA JUMA hili la 44 la mwaka 2019, tutakwenda kupata uchambuzi wa kina wa kitabu hiki, na kujifunza masomo hayo 15 na jinsi tunavyoweza kuyatumia na sisi kufanikiwa zaidi kwenye biashara zetu.

Makala ya TANO ZA JUMA, pamoja na uchambuzi mwingine wa vitabu na vitabu vyenyewe vinapatikana kwenye channel ya telegram inayoitwa TANO ZA JUMA, maelezo ya kujiunga na channel hii yako hapo chini. Karibu sana kwenye channel hii ujifunze kupitia vitabu mbalimbali.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu