Unapoteza muda wako kujifunza na kusoma vitabu, kama mwisho wa siku unaendelea na maisha yako kama yalivyokuwa kabla hujajifunza.

Lengo la kujifunza vitu vipya siyo kujua vitu hivyo vipya na kujisifia kwamba unajua sana.

Bali kutumia yale uliyojifunza kuweza kuwa bora zaidi. Hivyo ukishajifunza unapaswa kubadili maisha yako na kufanya kwa utofauti kile ambacho unafanya.

Kama utajifunza kitu kipya, halafu ukarudi kuishi au kufanya kama ulivyokuwa unafanya kabla hujajifunza, ulichojifunza hakijawa na msaada wowote kwako, na umepoteza muda wako.

Kazi yako kubwa siyo kufanya vitu leo kama ulivyofanya jana, huo ni mtazamo mbaya sana kwenye maisha, kazi na hata  biashara. Kazi yako kubwa ni kufanya vitu kwa namna iliyo bora kabisa kulingana na maarifa na taarifa tulizonazo sasa.

Hivyo unapopata maarifa na taarifa mpya, zitumie moja kwa moja kwa namna unavyofanya shughuli zako na kuendesha maisha yako.

Ndiyo maana nimekuwa nashauri kwa kila kitabu unachosoma, ondoka na kitu kimoja utakachokwenda kukifanyia kazi mara moja. Kwa kila semina unayoshiriki, ondoka na kitu kimoja unachokwenda kuanza kufanyia kazi.

Hivi ndivyo unavyoweza kunufaika kupitia yale unayojifunza kwenye maisha, kwa kuyatumia kwenye maisha yako ya kila siku.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha