Watu wengi wamekuwa wanafanya maamuzi mengi kwenye maisha yao, lakini hawayatekelezi, na hilo linawazuia wasipige hatua kwenye maisha yao.

Hii inatokana na tabia ya watu wengi kupenda kuyahoji na kuyapa changamoto maamuzi yao, hasa pale wanapokutana na ugumu katika kutekeleza maamuzi hayo.

Mtu anaamua kwamba ataingia kwenye biashara fulani, lakini wakati wa kuanza unapofika anaanza kujiuliza kama ndiyo biashara sahihi, kama ni biashara itakayomfaa, kama yupo tayari kuanza na mengine mengi.

Kwa njia hiyo, anajikuta ana sababu nyingi za kutokuanza na hivyo haanzi.

Kuondokana na hali hii, unapaswa kuyaheshimu maamuzi yako, unapofanya maamuzi, hakikisha unayatekeleza kama ulivyopanga, hata kama utakutana na sababu au vikwazo vya aina gani. Wewe fanya kama ulivyopanga na kwa namna ulivyopanga. Usibadili maamuzi yako kabla hujayafanyia kazi. Yabadili baada ya kuwa umefanyia kazi na kujifunza njia bora zaidi ya kufanya.

Hili ni muhimu sana, hata kama ni kwa mambo madogo kwa sababu linakujengea msimamo. Unapofanya maamuzi halafu usiyatekeleze, unajiambia wewe ni mtu ambaye hutekelezi maamuzi. Hivyo unajidharau na kila maamuzi utaishia kutokuyatekeleza. Unapofanya maamuzi na kisha ukayasimamia unajiheshimu, unajiambia wewe ni mtu unayesimamia maamuzi yako na hivyo ndivyo utakavyofanya mara zote.

Kumbuka hadithi tunazojiambia kila siku zina nguvu kubwa sana, na hadithi hizi zinatengenezwa na fikra tunazokuwa nazo na hatua tunazochukua. Anzia kwenye maamuzi yako, fanya maamuzi kwa usahihi na ukishaamua basi simamia mpaka maamuzi hayo mpaka upate kile ambacho unakitaka.

Usiwe mtu wa kufanya maamuzi halafu kuanza kupingana na maamuzi yako mwenyewe. Utajijengea uzembe ambao utakuwa kikwazo kwa mafanikio yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha