“Don’t trust in your reputation, money, or position, but in the strength that is yours—namely, your judgments about the things that you control and don’t control. For this alone is what makes us free and unfettered, that picks us up by the neck from the depths and lifts us eye to eye with the rich and powerful.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 3.26.34–35
Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi hii bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari NGUVU IPO KWENYE MATAKWA MACHACHE…
Wale wanaoanza safari ya mafanikio kwa mtazamo kwamba watakuwa na furaha wakishapata kila wanachotaka, wanakuja kugundua kwamba hilo ni lengo gumu sana kwao kufikia.
Kwa sababu kila wanapopata kitu kimoja, wanaona kuna kingine zaidi wanaweza kukipata, hivyo furaha inasogezwa mbele.
Mtu anapokuwa anatembea kwa mguu, anaweza kujiambia akipata baiskeli atafurahia maisha, anaipata ba kugundua pikipiki itakuwa bora zaidi kwake, maana anachoka kuchochea baiskeli.
Anapata pikipiki, na hapo anagundua wakati wa mvua ni vigumu sana kwake kufanya safari zake, hivyo anajiambia akipata hata kigari kidogo tu, atakuwa na furaha. Anapata kigari kidogo na akienda kupaki sehemu waliyopaki watu wengine, anagundua yeye pekee ndiye mwenye kigari kidogo, hivyo anahitaji gari kubwa zaidi.
Hivyo ndivyo watu wanavyoahirisha furaha kwenye maisha yao, hivyo ndivyo watu wanavyojinyima nguvu.
Njia pekee ya kuwa na furaha na hata nguvu na namlaka kwenye maisha yako siyo kupata kila unachotaka, bali kuwa na matakwa machache.
Kupata kila unachotaka ni kitu kisichowezekana, kwa sababu unapopata kitu kimoja unashawishika kutaka kitu kingine.
Lakini unapokuwa na matakwa machache, unapokuwa hujali sana kuhusu kile unachopata, unakuwa na maisha yenye uhuru, yenye nguvu na mamlaka na yenye furaha.
Endesha maisha yako kwa kuwa na matakwa machache,
Na hii haimaanishi kwamba usijitume na usitafute utajiri, badala yake ni kuondokana na tamaa ambazo huwezi kuzishibisha.
Endelea kujituma sana, endelea kupiga hatua kubwa, kwa sababu una kitu kikubwa ndani yako ambacho unataka kukitoa kwa dunia na siyo kwa sababu kuna matakwa yako unataka kuyatimiza.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa na matakwa machache na kujituma kwa ajili ya kutoa mchango wako kwa dunia na siyo kwa ajili ya kupata kila unachotaka.
#HuweziKuridhishaTamaa #KuwaNaMatakwaMachache #UsiwekeFurahaYakoKwenyeVitu
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1