“If we judge as good and evil only the things in the power of our own choice, then there is no room left for blaming gods or being hostile to others.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 6.41
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii mpya ambayo tumekuwa nayo leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari BEBA JUKUMU LA MAISHA YAKO…
Kuanzia leo, jiambie maisha yako ni jukumu lako.
Chochote kinachotokea au kutokutokea ni kwa sababu yako wewe.
Kwa maana hiyo, hakuna mtu yeyote anayepaswa kulalamikiwa au kulaumiwa kwa chochote kinachotokea kwenye maisha yako, ila wewe mwenyewe.
Wewe mwenyewe ndiye ambaye umejiweka kwenye hali uliyopo sasa, na kuchangia matokeo ambayo unayapata sasa.
Watu na vitu vingine vinaweza kuwa na mchango, lakini mzizi mkuu unaanzia kwako.
Kama watu wamekuibia, ni wewe umeanza kwa uzembe mpaka kutoa mwanya wa watu kukuibia.
Kama watu wamekutapeli, ni wewe umewapa nafasi kwa kuwaamini kabla hujajiridhisha kuhusu uaminifu wao.
Kama kazini hupandishwi cheo au kupewa fursa zaidi ni kwa sababu hujitumi vya kutosha kwenye kazi zako.
Kama biashara yako haiingizi faida nzuri, ni kwa sababu huweki juhudi za kutosha kupata wateja wapya na kuwapa huduma nzuri.
Kwa kila jambo au hali unayopitia, kuna namna ambavyo wewe mwenyewe umeitengeneza, wewe mwenyewe umechangia hali kuwa hivyo.
Hivyo basi, hupaswi kulalamika au kumlaumu yeyote kwa chochote kinachotokea kwenye maisha yako.
Badala yake jiulize umechangiaje kwenye hali hiyo, kisha chukua hatua sahihi ili kubadili hayo matokeo uliyoyapata.
Ukichagua kuyaendesha maisha yako kwa namna hii, utakuwa mtu wa kuchukua hatua na kusonga mbele na siyo mtu wa lawama na malalamiko.
Wanaofanikiwa ni wanaochukua hatua, wanaoshindwa ni wanaolalamika na kulaumu.
Chagua vizuri upande wako na utumikie vyema.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kubeba jukumu la maisha yako, kwa kujua kila kinachotokea kimesababishwa na wewe na siyo watu au vitu vingine. Hivyo kuchukua hatua sahihi na siyo kulalamika au kulaumu.
#BebaJukumuLaMaishaYako #LawamaHazijengi #ChukuaHatua
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1