Karibu kila mtu anajua nini anachotaka kwenye maisha yake.

Na katika hao, wengi wanajua nini wanapaswa kufanya ili wapate kile wanachotaka.

Lakini inapofika wakati wa kuchukua hatua, wengi huwa hawachukui hatua, kwa kuhofia kushindwa.

Na hili linawaweka watu kwenye hali mbili, majuto au makosa.

Majuto yanakuja pale ambapo mtu hajafanya kitu, anajua kabisa anachopaswa kufanya, lakini yeye anachagua kutokufanya. Hili linamfanya awe na majuto, kwa kujiambia kama ninge…

Makosa yanakuja pale ambapo mtu amefanya kitu na akakosea, kutokana na kutokujua au kutokuwa na uzoefu wa kutosha kwenye kitu hicho.

Watu wengi wamekuwa wanaogopa makosa na ndiyo maana hawachukui hatua, wanaona makosa yanaumiza sana hivyo ni bora wasubiri mpaka watakapokuwa tayari.

Lakini wasichojua ni kwamba, majuto huwa yanaumiza zaidi kuliko makosa. Kwa sababu majuto huwa yanadumu milele, lakini makosa huwa ni ya muda mfupi. Unapofanya makosa una nafasi ya kuyarekebisha na kuboresha zaidi. Lakini unapokuwa hujachukua hatua, utakuwa na majuto kwa wakati wote.

Ni bora kuchukua hatua na ukakosea, kuliko kutokuchukua hatua na ukajutia. Majuto yatakuumiza lakini hakuna ambacho unajifunza. Makosa yatakuumiza lakini yatakupa funzo kubwa, funzo la njia ipi siyo sahihi kutumia.

Kwa chochote ambacho umekuwa unaahirisha kufanya, amua leo kufanya hata kama hujawa tayari, kwa sababu hakuna siku ambayo utakuwa tayari. Ni bora ufanye, ukosee na ujifunze, kuliko kutokufanya, usikosee lakini ujutie.

Makosa yanaumiza kwa muda mfupi, majuto yanaumiza milele, kuwa mtu wa kufanya, usiogope makosa, hakuna asiyekosea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha