“He was sent to prison. But the observation ‘he has suffered evil,’ is an addition coming from you.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 3.8.5b–6a
Ni jambo la kushukuru sana kwa mimi na wewe kuipata zawadi hii nyingine nzuri ambayo ni kuiona siku hii ya leo.
Siyo kwa sababu tunastahili sana, au kwa sababu tu wajanja sana, ila ni kwa bahati tu.
Muda huu tulioupata ndiyo nafasi ya sisi kuwa bora zaidi, kufanya kwa ubora zaidi na kuzalisha matokeo bora zaidi.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari WEWE NDIYE UNAYECHAGUA MATOKEO…
Watu wanaweza kufanya chochote kile kwako, lakini hawana nguvu ya kuamua ni matokeo gani wewe uyapate.
Ni wewe pekee ndiye utakayeamua na kuchagua matokeo ya aija gani unayapata.
Mtu anaweza kukupiga au kukutukana, lakini ni wewe utakayeamua kama unaumia au umedharaulika au umemjua mtu kwa uhalisia wake.
Mtu anaweza kukuibia au kukutapeli, lakini ni wewe utakayeamua kama umeonewa au umejifunza tabia halisi za watu.
Kwa kila kinachotokea kwenye maisha yetu, tunayo nguvu kubwa ya kuchagua, kama tunakuwa upande wa wanyonge au upande wa washindi.
Hakuna chochote ambacho kinakutokea na usiweze kukigeuza kuwa ushindi kwako.
Ni wewe tu kuchagua.
Wengi waliofanikiwa walipitia magumu ambayo walioshindwa walipitia pia.
Kilichowatofautisha ni namna ambavyo walichukulia magumu hayo.
Kama utayachukulia magumu kama sehemu ya wewe kuwa imara na kufikia ushindi zaidi, hutabaki pale ulipo sasa.
Lakini kama utayatumia magumu kama sababu ya kushindwa na kulalamika, hutatoka pale ulipo sasa.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuchagua matokeo sahihi kwako, ambayo yatakutoa pale ulipo sasa na kukufanya kuwa bora zaidi ya ulivyo sasa. Chaguw matokeo chanya, chagua matokeo ya ushindi.
#UnachaguaMatokeo #ChaguaUpandeChanya #UshindiNiWako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1