“Hecato says, ‘cease to hope and you will cease to fear.’ . . . The primary cause of both these ills is that instead of adapting ourselves to present circumstances we send out thoughts too far ahead.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 5.7b–8

Kuiona siku hii nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu ni jambo la kushukuru sana.
Wapo wengi ambao walipenda sana kuiona siku hii, lakini hawajapata bahati kama tuliyoipata sisi.
Wapo wengine ambao wangekuwa tayari kulipa mamilioni ya fedha ili kuiona siku hii, lakini haijawezekana.
Lakini mimi na wewe, bila ya kulipa jata senti moja, tumepewa tena siku hii mpya ya leo.
Kama tutachagua kuipoteza kwa kutumia muda wetu vibaya, basi tutakuwa tumefanya jambo la hovyo mno.
Tukaiishi siku hii ya leo kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA, mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA pamoja na msimamo wa KAZI, UPENDO NA HUDUMA.

Asubuhi ya leo tutafakari MATUMAINI NA HOFU NI KITU KIMOJA…
Matumaini huwa yanachukuliwa kama kitu kizuri.
Watu wanapokuwa na matumaini, wanapata msukumo wa kwenda zaidi hata pale mambo yanapoonekana magumu.
Watu wanapokosa matumaini, wanakata tamaa.
Hofu ni kitu kibaya, hofu ndiyo inawazuia wengi kupiga hatua, hofu ndiyo inawafanya wengi kubaki pale walipo sasa.
Hivyo tunaambiwa tuwe na matumaini lakini tuepuke kuwa na hofu au tuishinde hofu.

Lakini wastoa wana habari ya kutushtua na kutushangaza kidogo, wanatuambia matumaini na hofu ni kitu kimoja.
Wanatuambia matumaini na hofu vyote ni matarajio ya vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wetu.
Vyote ni maadui wa kuishi kwenye muda ambao tunao sasa,
Badala ya kuchukua hatua kwenye hali unayopitia sasa, matumaini yanakufanya uone siku zijazo zitakuwa bora zaidi na hofu inakufanya usichukue hatua yoyote kwa sasa.

Hatari nyingine ni kwamba, unapojiwekea matumaini unazalisha hofu pia. Kila unapofikiria kwamba mambo yatakuwa mazuri zaidi baadaye, unapata mawazo ya vikwazo vinavyoweza kuzuia mambo yasiwe mazuri kama unavyopanga, na hapo unaikaribisha hofu.
Ukiacha kuweka matumaini, utaondokana na hofu kabisa.

Lakini je tutaishije bila ya matumaini, nini kitatupa msukumo wa kuendelea kupambana hata pale mambo yanapoonekana magumu?
Jibu ni moja, kuishi msingi wa ustoa unaojulikana kama amor fati ambao ni kuipenda asili, kupokea kila kinachokuja kwako na kukitumia kwa wakati ulionao.
Badala ya kutaka mambo yaende kama unavyotaka wewe, kitu amnacho kipo nje ya uwezo wako, unachagya kupokea kila kinachotokea na kukitumia vizuri.
Kwa namna hii utaishi kwenye wakati uliopo na kuacha kutengeneza matumaini ambayo yanakujengea hofu pia.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuacha kuishi kwa matumaini na hofu na badala yake kupokea kila ambacho asili inakileta kwako na kisha kukitumia vizuri.
#MatumainiSiyoMkakati #HofuInatengenezwa #IpendeAsili

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1