Watu waliofanikiwa wanatumia vitu, watu walioshindwa wanatumiwa na vitu. Ni tofauti moja ndogo sana lakini yenye madhara makubwa kwenye maisha ya mtu.

Watu waliofanikiwa wanatumia fedha kufanya yale muhimu na hivyo kuweza kufanikiwa zaidi na kutengeneza maana kwenye maisha yao. Wakati wale walioshindwa wanatumiwa na fedha, wakiwa nazo wanajikuta wanafanya mambo ambayo hawajui kwa nini wameyafanya.

Watu waliofanikiwa wanatumia muda kwa kuupangilia vizuri na kuweka vizuri vipaumbele vyao. Kwa upande wa pili, wale walioshindwa wanatumiwa na muda, wanajikuta wana muda na hawajui wafanye nini, kinachotokea ni wanapoteza muda huo na kushindwa kupiga hatua yoyote kubwa kwenye maisha yao.

Kutumia na kutumiwa ni kipimo sahihi cha kiwango cha udhibiti na uhuru ambacho mtu anacho kwenye maisha yake na kila anachofanya. Hivyo unaweza kujipima wewe kwa kila eneo la maisha yako, je unatumia au unatumiwa.

Mfano mzuri ni kwenye watu, watu waliofanikiwa wanatumia watu kuwasaidia kufikia ndoto zao kubwa. Lakini wale walioshindwa huwa wanatumiwa na watu wengine kuwasaidia watu hao kufanikiwa zaidi.

Unatumia au unatumiwa? Hili ni swali muhimu la kujiuliza kwenye kila eneo la maisha yako, kwa kila unachofanya na hata unachomiliki.

Kama upo upande wa kutumiwa, ni wakati sasa wa kuchukua hatua na kuanza kutumia. Ukitumiwa unachoka na hupigi hatua, ukitumia unapata nguvu na kupiga hatua. Mara zote chagua kutumia na siyo kutumiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha