Kwenye safari ya mafanikio, hakuna mwalimu mbaya kujifunza kwake kama mafanikio yako ya nyuma, na hata ya wengine.

Ni bora kujifunza kutoka kwenye kushindwa kwako au kwa wengine, utapata mafunzo mazuri kuliko kujifunza kutoka kwenye mafanikio.

Mafanikio ni mwalimu mbaya kwa sababu ni vigumu sana kujua chanzo halisi cha mafanikio. Mafanikio yoyote yale yanakuwa yamehuisha vitu vingi, siyo tu kuweka juhudi na maarifa, lakini pia kuna bahati ambazo zinahusika, au kuwa kwenye eneo sahihi kwa wakati sahihi.

Unaweza kufanikiwa kwenye jambo moja, na ukarudia kile kile ulichokifanya kwenye jambo jingine na ukashindwa vibaya sana. Ndiyo maana wale waliofanikiwa kwenye biashara moja wanapojaribu kwenda kuanza biashara nyingine ya tofauti huwa wanashindwa vibaya.

Kushindwa ni mwalimu mzuri, kwa sababu ni rahisi kuona chanzo cha kushindwa. Mara zote kushindwa kunatokana na maamuzi au hatua mbovu ambazo mtu anakuwa amechukua, unaweza kuziona kwa urahisi na kutokuzirudia tena.

Hata ukiwaangalia wale walioshindwa, unaona wazi ni wapi waliposhindwa, hivyo ukiepuka kufanya kile ambacho wao wamefanya, utajiepusha kushindwa kama wao.

Weka juhudi kupata ushindi na mafanikio, lakini unapofanikiwa kuwa mnyenyekevu, kuna vitu vingi vimechangia mafanikio yako ambavyo huenda huvijui. Hivyo usifikiri tayari unajua kila kitu kuhusu mafanikio, lazima uendelee kujifunza kila siku, hasa kupitia makosa yako na ya wengine pia.

Mafanikio ni mazuri kuwa nayo, lakini ni mwalimu mbaya kwako, angalia yasije kukupoteza pale unapoyapata au kuyaangalia kwa wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha