Umeambiwa kuna tamthilia nzuri imetoka, kila mtu anaisifia, unapata shauku ya kwenda kuiangalia.
Unakwenda kuiangalia, na hivi ndivyo inavyokwenda. Mwigizaji mkuu kwenye tamthilia hiyo, anazaliwa kwenye maisha ya utajiri, anasoma shule nzuri na kufaulu vizuri, anapata kazi nzuri, anakuwa na mke na familia nzuri anaishi maisha yake vizuri na kisha kufariki.
Hebu niambie tamthilia hiyo imekuwa nzuri kwako kuangalia? Kwamba mwigizaji mkuu hajapitia ugumu wowote ule, maisha yake yamekwenda kama alivyopanga na kila alichotaka amekipata. Utapata msukumo wa kuendelea kuangalia tamthilia hiyo? Au kurudia tena kuiangalia?
Jibu ni hapana, hutaipenda tamthilia hiyo, haitakuvutia.
Tamthilia tunazopenda kuangalia ni zile ambazo mwigizaji mkuu anapitia magumu mengi, ambayo ni makubwa lakini anapambana na kuyashinda. Kuna wakati mpaka wewe mtazamaji unaona hapo ndiyo mwisho wake, hawezi tena, lakini anaweza, na hilo linakufanya uipende kweli tamthilia hiyo.
Saa cha kushangaza, inapokuja kwenye maisha yako, unataka aina ya kwanza ya tamthilia, unataka kila kitu kiende kama unavyotaka wewe, unataka usikutane na magumu yoyote, mambo yawe mteremko. Hivi unafikiri maisha hayo yatakuwa na uzuri wa kuyaishi?
Kama ambavyo hutapenda kuangalia tamthilia ambayo mwigizaji mkuu hakutani na magumu, ndivyo ambavyo hutayapenda maisha ambayo hayana changamoto yoyote. Utajikuta unatafuta vitu vingine vya kukusumbua.
Changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha ndiyo zinazoyafanya maisha yetu kuwa na maana. Ni magumu hayo ndiyo yanatengeneza hadithi ya maisha yako, ndiyo yanakusukuma ufanye makubwa zaidi.
Usiyakimbie magumu ya maisha, usiyaogope, badala yake yakaribishe na yatumie kukufanya kuwa bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,